• HABARI MPYA

  Alhamisi, Januari 29, 2015

  KOPUNOVIC ATAJA SABABU TOSHA SIMBA KUCHAPWA NA MBEYA CITY JANA, ASEMA WACHEZAJI WAMELEWA SIFA ZA MAPINDUZI, ‘VIBEGA JUU’

  Na Princess Asia, DAR ES SALAAM
  KOCHA Mkuu wa Simba SC, Mserbia Goran Kopunovic amesema kwamba kuwakosa nyota wake, beki Hassan Kessy, kiungo Said Ndemla na mshambuliaji Emmanuel Okwi kulichangia kipigo cha jana kutoka Mbeya City.
  Simba SC ilifungwa mabao 2-1 na Mbeya City Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara na Mserbia huyo alizungumza na Waandishi wa Habari juu ya kipigo hicho.
  Kocha wa Simba SC, Goran Kopunovic ameelezea sababu za timu yake kupoteza mchezo wa jana dhidi ya Mbeya City 
  Pamoja na kusema kwamba kuwakosa majeruhi Kessy, Ndemla na Okwi kulichangia, lakini pia Kopunovic alisema kwamba hata timu yake jana haikucheza vizuri kipindi cha pili.
  Alisema anadhani wachezaji wake wameanza kujiona mastaa baada ya mafanikio kidogo hivyo kupoteza malengo mapema na kwa upande mwingine anakifurahia kipigo cha jana, akiamini kitawazindua wachezaji wake. 
  Katika mchezo huo, Simba SC ilipata nafasi ya kutoa sare baada ya kupewa penalti, dakika ya mwisho, lakini beki Nassor Masoud ‘Chollo’ akaenda kugongesha mwamba wa juu.
  “Sina mchezaji maalum wa kupiga penalti hadi sasa, na ilipotokea tumepata penalti, nikawaambia wachezaji yeyote anayejiona anaweza kuiokoa timu, akapige. Lakini nilishangaa Chollo kwenda kupiga, kwa sababu sijawahi kumuona akipiga penalti tangu nimefika hapa,”alisema Kopunovic.
  Hata hivyo, Mserbia huyo alisema hawezi kumlaumu sana Chollo, bali lawama zake ni kwa timu nzima namna walivyocheza vibaya dakika 30 za mwisho.
  “Hii ligi ni ngumu, japokuwa tuliwafunga Ndanda (2-0) na tukacheza vzuri tukitoka sare (1-1) na Azam, lakini ligi hii ni ngumu. Naona wachezaji wameanza kujisahau, sasa wataamka, wanatakiwa kuongeza juhudi na kujipanga kwa mapambano zaidi kama tunataka kufanya vizuri katika ligi,”amesema.
  Amesema wachezaji wake wanatakiwa kusahau mafanikio ya nyuma, kama kutwaa Kombe la Mapinduzi mapema mwezi huu visiwani Zanzibar na kuelekeza nguvu zao kikamilifu katika kupigania ubingwa wa Bara.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: KOPUNOVIC ATAJA SABABU TOSHA SIMBA KUCHAPWA NA MBEYA CITY JANA, ASEMA WACHEZAJI WAMELEWA SIFA ZA MAPINDUZI, ‘VIBEGA JUU’ Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top