• HABARI MPYA

    Saturday, January 24, 2015

    AZAM FC KUMKOSA AISHI MANULA KESHO DHIDI YA SIMBA SC, BOCCO TAYARI KUCHINJA ‘MNYAMA’ TAIFA JUMAPILI

    Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
    AZAM FC itamkosa kipa wake hodari, Aishi Manula katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara dhidi ya Simba SC kesho Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
    Kipa huyo chipukizi mwenye kipaji na uwezo wa hali ya juu, atakuwa anatumikia adhabu ya kadi tatu za njano kesho, na maana yake Azam FC itabaki na kipa mmoja tu mzoefu, Mwadini Ali.
    Kipa wa tatu wa Azam FC, Jackson Wandwi pamoja na kuonyesha uwezo mkubwa mazoezini siku zote hajawahi kuaminiwa katika mechi za mashindano.
    Lakini habari njema tu kwa wapenzi wa Azam FC ni kwamba, mshambuliaji kiboko ya vigogo, John Raphael Bocco ‘Adebayor’ yuko kambini tayari kwa mchezo huo.
    Aishi Manula anatumikia kadi tatu za njano, hatakuwepo kesho Azam FC ikimenyana na Simba SC

    Bocco mwenye ngekewa ya kuzifunga Simba na Yanga hata ‘akiamshwa usingizini’ hakuwepo katika mechi mbili zilizopita za Azam FC, dhidi ya Stand United mjini Shinyanga na Kagera Sugar mjini Mwanza kwa sababu alikwenda Algeria kufanya mipango ya kujiunga Chabab Riadhi Baladiyat, maarufu kama CRB. 
    Azam FC ilishinda mechi zote za Kanda ya Ziwa bila Bocco, 1-0 dhidi ya Stand bao pekee la kiungo Frank Domayo na 3-1 dhidi ya Kagera Sugar mabao mawili ya Didier Kavumbangu na moja la Kipre Tchetche.
    Hata hivyo, Bocco alirejea mwishoni mwa wiki Dar es Salaam baada ya kushindwa kufikia makubaliano na klabu hiyo inayovalia jezi za rangi nyeusi na nyeupe, ambayo inashiriki Ligi Daraja la Kwanza Algeria, maarufu kama Professionnelle 2.
    John Bocco kushoto yuko tayari kuendeleza desturi yake ya kuifunga Simba SC kesho

    Hii inakuwa mara ya tatu kwa Bocco kujaribu bila mafanikio kuhamia nje, baada ya awali kufanya majaribio Afrika Kusini na Israel, ambako licha ya kuelezwa alifuzu, lakini biashara haikufanyika.
    Awali, Bocco alifanya majaribio kwa wiki kadhaa katika klabu ya Ligi Kuu Israel mwaka 2010 na baadaye Afrika Kusini katika klabu ya Supersport United.
    Bocco alifuzu Supersport baada ya wiki mbili, lakini Azam FC ikagoma kumuuza kwa sababu ya dau dogo.
    Meneja wa Azam FC, Jemadari Said Kazumari amesema kwamba pamoja na kwamba watamkosa Aishi, lakini wana imani na makipa waliobaki, Mwadini na Wandwi.
    Kwa ujumla Jemadari amesema kikosi kipo vizuri kuelekea mchezo huo na hakuna shaka watabeba pointi tatu mbele ya Wekundu wa Msimbazi Jumapili.
    Azam FC ipo kileleni mwa Ligi Kuu kwa sasa kwa pointi zake 20 baada ya kucheza mechi 10, ikifuatiwa na Mtibwa Sugar yenye pointi 17 za mechi tisa, wakati Simba SC ina pointi 12 za mechi tisa. 
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: AZAM FC KUMKOSA AISHI MANULA KESHO DHIDI YA SIMBA SC, BOCCO TAYARI KUCHINJA ‘MNYAMA’ TAIFA JUMAPILI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top