• HABARI MPYA

    Saturday, January 31, 2015

    SSERUNKUMA ATULIZA UPEPO SIMBA SC, APIGA ZOTE MBILI MNYAMA AKIITAFUNA JKT RUVU

    Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
    MABAO mawili ya mshambuliaji wa kimataifa wa Uganda, Dan Sserunkuma jioni ya leo yametuliza hali ya hewa Msimbazi, baada ya Simba SC kuibuka na ushindi wa 2-1 dhidi ya JKT Ruvu Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
    Hamkani ilianza kuwa si shwari ndani ya Simba SC, baada ya kipigo cha mabao 2-1 pia katika mchezo uliopita wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara mbele ya Mbeya City Uwanja wa Taifa, lakini Sserunkuma ameweka mambo sawa.
    Katika mchezo huo uliochezeshwa na refa Ofisa wa jeshi la Polisi, Hashim Abdallah wa Dar es Salaam, aliyesaidiwa na Rashid Zongo wa Iringa na Abdallah Shaka wa Tabora, hadi mapumziko kila timu ilikuwa imekwishapata bao moja.
    Ibrahim Hajib kushoto akimpongeza Dan Sserunkuma baada ya kuifungia Simba SC mabao mawili leo

    Simba SC ndiyo waliokuwa wa kwanza kupata bao lililofungwa na Dan Sserunkuma, aliyemaliza pasi ya Mganda mwenzake, Emmanuel Okwi kutokea pembeni kulia.
    JKT Ruvu walisawazisha bao hilo kupitia kwa George Minja dakika ya aliyeunganisha kwa kichwa kona ya Ramadhani Haruna Shamte.
    Kipindi cha pili, Simba SC ilikianza vizuri na dakika ya pili tu, Sserunkuma tena kwa usaidizi mzuri wa Okwi akaipatia timu yake bao la pili ambalo linakuwa nao lake la tatu katika ligi tangu asajiliwe Desemba kutoka Gor Mahia ya Kenya.
    Simba SC ilipoteza nafasi tatu nzuri za kufunga baada ya hapo, wote Okwi, Dan Sserunkuma na Simon Sserunkuma aliyetokea benchi wakiwa wamebaki na kipa Benja Haule wakakosa mabao.
    Dan Sserunkuma akimiliki mpira mbele ya mabeki wa JKT Ruvu leo
    Emmanuel Okwi akimtoka beki wa JKT Ruvu, Ramadhani Haruna Shamte

    Ushindi huo, unaifanya SImba SC ifikishe pointi 16 baada ya mechi 12 na kujiondoa nafasi za mkiani.  
    Kikosi cha Simba SC kilikuwa; Ivo Mapunda, Kessy Ramadhani, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’, Hassan Isihaka, Juuko Murshid, Jonas Mkude, Ramadhani Singano ‘Messi’, Abdi Banda/Awadh Juma dk87 , Dan Sserunkuma, Ibrahim Hajibu/Simon Sserunkuma dk67 na Emmanuel Okwi.
    JKT Ruvu; Benjamin Haule, Ramashan Shamte, Napho Zuberi, Renatus Morris, Mohammed Faki, George Minja, Ally Bilal/Issa Kandulu dk67, Nashon Naftal/Amos Mgisa dk12, Samuel Kamuntu, Iddi Mbaga/Najim Magulu dk46 na Jabir Aziz.  
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: SSERUNKUMA ATULIZA UPEPO SIMBA SC, APIGA ZOTE MBILI MNYAMA AKIITAFUNA JKT RUVU Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top