• HABARI MPYA

  Friday, January 23, 2015

  KEVIN FRIDAY: NILICHEZA NINAUMWA

  Na Mwandishi Wetu, MWANZA
  MFUNGAJI wa bao la kusawazisha la Tanzania jana katika sare ya 1-1 na Rwanda katika mchezo wa kimataifa wa kirafiki Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza, Kevin Friday amesema alicheza anaumwa.
  “Nimecheza ninaumwa, mwalimu alikuwa anajua hilo, lakini akaniambia nijitahidi nicheze kidogo, nikishindwa atanitoa, ndiyo maana kwa kweli jana sikuwa katika kiwango changu,”amesema Friday akizungumza na BIN ZUBEIRY jana mjini hapa.
  Hata hivyo, Friday alisema baada ya Rwanda kupata bao la kuongoza, alilazimika kujituma zaidi hadi akafanikiwa kuifungia bao la kusawazisha Taifa Stars Maboresho.
  Kevin Friday aliifungia bao pekee Taifa Stars Maboresho jana katika sare ya 1-1 na Rwanda, hapa anashangilia na Said Ndemla

  “Na nilipofunga tu, nikahisi kama homa yote imetoka na damu ikaanza kuchemka, nilijiona mwepesi tangu pale, na nikaona kabisa sasa ninacheza inavyotakiwa,”alisema.  
  Timu ya vijana chini ya umri wa miaka 23, maarufu kama Taifa Stars Maboresho, jana ilitoka sare ya kufungana bao 1-1 na Rwanda katika mchezo wa kirafiki uliofanyika Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza.
  Licha ya kuundwa na wachezaji vijana wadogo, lakini timu ya Mholanzi, Mart Nooij ilicheza soka ya kuvutia, hususan kipindi cha pili dhidi ya Rwanda iliyoundwa na wazoefu, wakiwemo wachezaji wa kulipwa. 
  Hadi mapumziko, timu hizo zilikuwa zimekwishafungana bao 1-1, Rwanda wakitangulia dakika ya tisa na Tanzania kusawazisha dakika ya 44.
  Bao la Rwanda lilifungwa na Jean Baptiste Mugiraneza kwa kichwa akiunganisha krosi ya Emery Bayisenga aliyemtoka Gardiel Michael.
  Tanzania walisawazisha kupitia kwa Kevin Friday dakika ya 44 aliyefumua shuti kali nje kidogo ya 18 baada ya kupata pasi nzuri ya kichwa ya Simon Msuva, ambaye naye alipokea pasi ya Miraj Adam.
  Rwanda inayofundishwa na kocha wa muda, Muingereza Lee Johnson ambaye ni Mkurugenzi wa Ufundi wa FERWAFA, ilitawala mchezo kipindi cha kwanza na ilionekana kama Tanzania ingefungwa mabao zaidi, lakini uimara wa safu ya ulinzi iliyoongozwa na kipa Peter Manyika ulisaidia.
  Kipindi cha pili, Stars Maboresho iliimarika zaidi na kuuteka mchezo, ikipeleka mashambulizi mfululizo langoni mwa Rwanda, kiasi cha kukosa mabao mawili ya wazi.
  Mashabiki zaidi ya 15,000 waliojitokeza Uwanja wa CCM Kirumba wakiongozwa na Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Jamal Malinzi kwa ujumla walionekana kufurahishwa na kiwango cha timu hiyo, inayoandaliwa kwa ajili ya mechi za kufuzu za CHAN.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: KEVIN FRIDAY: NILICHEZA NINAUMWA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top