• HABARI MPYA

  Saturday, January 24, 2015

  KOPUNOVIC AMSIMIKA RASMI HASSAN ISIHAKA ‘UBOSI’ WA WACHEZAJI WENZAKE, MSAIDIZI WAKE JONAS MKUDE

  Na Princess Asia, DAR ES SALAAM
  KOCHA Mserbia, Goran Kopunovic amemkabidhi rasmi beki chipukizi, Hassan Isihaka Unahodha wa klabu ya Simba SC, wakati kiungo Jonas Mkude atakuwa Msaidizi wake.
  Kopunovic amefanya uteuzi huo jana baada ya mazoezi ya muda mfupi Uwanja wa Boko Veterani, nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam.
  Na anafanya uteuzi huo, kuelekea mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara dhidi ya mabingwa watetezi, Azam FC kesho.
  Pamoja na kuteua Manahodha hao wote walioibuliwa katika mfumo wa soka ya vijana ya klabu, Kopunovic pia ameteua jopo maalum la ‘watu wazima’ kama viongozi wa wachezaji wenazo.
  Hassan Isihaka alikuwa Nahodha wa Simba kwa majaribio wakati wa Kombe la Mapinduzi na akainua taji

  Hao ni kipa Ivo Mapunda, beki Nassor Masoud ‘Chollo’ na mshambuliaji Mganda, Emmanuel Okwi ambao jukumu lao litakuwa kuwaongoza wachezaji wenzao, ambao wengi wao ni vijana wadogo.
  Aliyekuwa Nahodha wa timu hiyo, beki wa kati pia, Joseph Owino kwa sasa amesusa kwa madai ametofautiana na kiongozi mmoja wa juu wa klabu hiyo na kuamua kurejea kwao Uganda na Isihaka alianza kuvaa beji katika michuano ya Kombe la Mapinduzi Januari akiiwezesha timu kutwaa Kombe.
  Simba SC watamenyana na Azam FC kesho Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam katika mfululizo wa Ligi Kuu, huo ukiwa mchezo wa pili kwa kocha huyo Mserbia tangu aanze kazi Msimbazi Januari akirithi mikoba ya Mzambia Patrick Phiri aliyefutwa kazi Desemba.
  Phiri alifutwa kazi baada ya kuambulia ushindi wa mechi moja tu kati ya nane, sita akitoa sare na moja kufungwa- wakati Kopunovic baada ya kuanza kwa kushinda mechi tano mfululizo na kubeba Kombe la Mapinduzi visiwani, Zanzibar, alifanikiwa kuanza vizuri pia katika Ligi Kuu kwa ushindi wa 2-0 dhidi ya wenyeji Ndanda FC ya Mtwara.
  Hivyo mchezo wa kesho unatarajiwa kuwa mtihani mzuri kwake, ambao utasaidia kuonyesha picha ya Simba ya baadaye chini ya mwalimu huyo wa zamani wa Polisi ya Rwanda. 
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: KOPUNOVIC AMSIMIKA RASMI HASSAN ISIHAKA ‘UBOSI’ WA WACHEZAJI WENZAKE, MSAIDIZI WAKE JONAS MKUDE Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top