• HABARI MPYA

  Wednesday, January 28, 2015

  WAPINZANI WA YANGA SC AFRIKA WALETA ‘JANJA YA NYANI’

  Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
  KLABU ya BDF XI inaonekana kuicheza shere Yanga SC, ili izembee maandalizi ya mchezo wa Raundi ya Awali ya Kombe la Shirikisho la Soka Afrika (CAF).
  Habari zimevuja kutoka ndani ya timu hiyo ya jeshi, kwamba haina uwezo wa kifedha kumudu gharama za kujilipia hoteli watakapokuja Dar es Salaam kwa ajili ya mchezo wa kwanza wiki ya pili ya mwezi ujao.
  Na habari hizo zimefika Yanga SC ambao wamezipokea kwa furaha, kiasi cha kuonekana kama kulegeza maandalizi yao.
  Lakini uchunguzi uliofanywa na BIN ZUBEIRY ikiwa ni pamoja na kuzungumza na maofisa wa BDF na Shirikisho la Soka Botswana, umebaini kuwa timu hiyo ya jeshi la nchi hiyo haijajitoa.

  Baada ya Shirikisho la Soka Afrika (CAF) kuagiza kila timu ijilipie gharama za hoteli katika mechi za ugenini, timu nyingi barani zilionekana kuumizwa na sheria hiyo mpya.
  Vyombo vya habari vya Botswana viliandika BDF nayo imeumizwa na sheria hiyo mpya na kuna uwezekano isiweze kuja Dar es Salaam kumenyana na Yanga SC.
  Lakini hiyo ni timu inayomilikiwa na Jeshi la nchi- haiyumkuniki ikakosa fedha za kulipia hoteli Dar es Salaam. 
  Serikali ya Botswana chini ya Rais Luteni Jenerali Seretse Ian Khama inayopenda michezo, haina umasikini wa kiasi hicho.
  Maofisa wawili wa BDF waliohojiwa na BIN ZUBEIRY kuanzia mwishoni mwa wiki wote walisema wanazisikia tu taarifa za timo yao kutoshiriki mashindano, na hawajui zinatoka wapi.
  Mkurugenzi wa Mashindano wa Shirikisho la Soka Botswana, Stephen Maleka aliiambia BIN ZUBEIRY jana kwamba, wao wanajua BDF XI itasafiri kwenda Tanzania wakati ukifika.
  “Kama kunakuwa na kitu kama hicho, sisi watu wa Shrikisho ndiyo tuwanaandika barua CAF na shirikisho la soka la Tanzania kuwataarifu,”alisema.
  Mwishoni mwa wiki, vyombo vya habari nchini viliripoti kwamba, Yanga SC watafuzu bila jasho Raundi ya Awali, kutokana na wapinzani BDF kujitoa.
  Na tangu taarifa hizo, Yanga haionekani kutotilia mkazo maandalizi yake. 
  Wawakilishi wengine wa Tanzania katika michuano ya Afrika, Azam FC wapo Lubumbashi, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) kwa kambi fupi ya wiki moja, ambayo itahusu mechi tatu za kujipima nguvu dhidi ya TP Mazembe, Don Bosco na ZESCO Unted ya Zambia. 
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: WAPINZANI WA YANGA SC AFRIKA WALETA ‘JANJA YA NYANI’ Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top