• HABARI MPYA

  Thursday, January 29, 2015

  MWAMBUSI AFICHUA ‘UCHAWI’ ALIOTUMIA KUUA MNYAMA

  Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
  KOCHA wa Mbeya City, Juma Mwambusi amesema kwamba mabadiliko ya kikosi chake aliyoyafanya kipindi cha pili jana ndiyo yaliimaliza Simba SC jana.
  Mbeya City ilitoka nyuma kwa bao 1-0 na kushinda 2-1 dhidi ya wenyeji Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara.
  Na baada ya kurudi vymba vya kubadilishia nguo wakiwa nuyma kwa 1-0, kipindi cha pili Mbeya City walibadilika na kuipeleka puta Simba SC hadi kupata ushindi huo.
  “Namshukuru Mungu kwa ushindi huu na pia nawapongeza vijana wangu kwa kazi nzuri, kwa sababu baada ya kuwa nyuma hadi mapumziko, nilizungumza nao, nikawaelekeza cha kwenda kufanya. Pamoja na mabadiliko niliyoyafanya, mambo yakawa mazuri tumechukua pointi tatu ugenini,”amesema Mwambusi.
  Juma Mwambusi akiwajibika jana Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam
      

  Simba SC wangeweza kupata sare ya 2-2 kama si beki Nassor Masoud ‘Chollo’ kukosa penalti dakika ya mwisho.
  Chollo alipiga penalti hiyo ikagonga mwamba wa juu dakika ya 90+3 baada ya beki Yussuf Abdallah kumchezea rafu kiungo Jonas Mkude kwenye boksi.
  Chollo alifanya kosa hilo, Simba SC ikitoka kufungwa bao la pili kwa penalti pia na Yussuf Abdallah baada ya kipa Peter Manyika kumshika miguu Raphael Daudi dakika ya pili 90+2.  
  Katika mchezo huo uliochezeshwa na refa Abdallah Kambua wa Shinyanga aliyesaidiwa na Anold Bugado wa Singida na Yahya Ali wa Mara, hadi mapumziko tayari Simba SC walikuwa mbele kwa bao 1-0.
  Bao hilo lilifungwa na mshambuliaji chipukizi, Ibrahim Salum Hajib dakika ya 45+2 kwa shuti la mpira wa adhabu kutoka umbali wa mita 20, baada ya kiungo Awadh Juma kuchezewa rafu.
  Mbeya City ilisawazisha bao hilo kupitia kwa Hamad Kibopile dakika ya 77 akitumia vizuri makosa ya mabeki wa Simba SC kuchanganyana na kipa wao, Peter Manyika.
  Mwambusi jana aliwaanzisha David Burhan, Richard Peter, Hamad Kibopile, Juma Nyosso, Yussuf Abdallah, Steven Mazanda, Themi Felix aliyempisha Hamidu Mohammed dakika ya 70, Raphael Alpha, Paul Nonga, Cossmas Freddy aliyempisha Peter Mapunda dakika ya 67 na Deus Kaseke aliyempisha Idrisa Rashid dakika ya 78.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: MWAMBUSI AFICHUA ‘UCHAWI’ ALIOTUMIA KUUA MNYAMA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top