• HABARI MPYA

  Monday, January 26, 2015

  BADILIKA BANZA STONE SOKO BADO LINAKUHITAJI SANA

  Niliwahi kuandika huko nyuma kuwa Banza Stone ni kama kisheti – anakwisha na utamu wake …kisheti utamu wake huwa ni ule ule mwanzo hadi mwisho, kisheti sio kama Big G ambayo sekunde kadhaa baada ya kuiweka kinywani utamu wote hutoweka.
  Banza bado anakubalika licha ukame wake wa kutokuwa na nyimbo nzuri kwa muda mrefu, wimbo wake  wa maana wa mwisho ni “Mtu Pesa alioutoa mwaka 2004 akiwa na Twanga Pepeta, nyimbo kama “Hujafa Hujasifika aliouachia miaka miwili baadae kupitia bendi ya Twanga Chipolopolo, haukushika chati kivile, hata wimbo wake wa “Watu na Falsafa” alioutunga ndani ya Extra Bongo miaka michache iliyopita, haukusumbua hata kidogo.

  Lakini bado Banza anaendelea kukubalika, akisimama jukwaani na kutupia vipande vya nyimbo kama “Kumekucha”, “Aungurumapo Simba”, “Mtaji wa Masikini”, “Elimu ya Mjinga” hakuna ambaye hatapagawa, labda awe kiziwi.
  Hakuna ubishi kuwa Ramadhani Masanja “Banza Stone” uwezo wake wa kughani sauti za juu umepotea, mwili wake umepoteza ung’aavu lakini bado anaposimama jukwaani heshima yake iko pale pale.
  Akishashika kipaza sauti watu watapagawa kwa namna yeyote alivyo, hawatajali iwapo sauti inapotea katikati ya nyimbo, wala hawatajali mwendo wake wa kuyumba yumba unaotokana na ‘kilaji’.
  Siku ya Idd Pili (mwezi Agust mwaka 2013) pale Mango Garden na hata siku ya Idd Tatu ndani Leaders Club, Banza Stone alipanda kwenye jukwaa la Twanga na kuimba nyimbo mbili “Mtu Pesa” na “Kumekucha” akashindwa kuzitendea haki lakini bado alishangiliwa.
  Banza alishindwa ‘kuudhibiti’ wimbo wa “Mtu Pesa”  - kuna sehemu zilikuwa zinamshinda na ikabidi Ige Moyaba ambaye alikuwa msanii mwalikwa awe na kazi moja ya kumdaka juu kwa juu kwenye uimbaji ili kuficha udhaifu uliojitokeza.
  Hata kwenye maonyesho ya enzi zake za Extra Bongo Banza alikuwa akipata shida anapoimba ile “Mega Mix” yake yenye mchanganyiko wa vipande vya nyimbo zake zilizopata umaarufu katika bendi mbali mbali alizozitumikia, kuna wakati alikuwa akishindwa kabisa kuimba baadhi ya vipande na ikawa inabidi kazi hiyo ifanywe na Ally Chocky.
  Kinachoonekana kwa sasa ni kwamba Banza Stone hana uwezo wa kudumu wa kuzitendea haki nyimbo zake majukwaani (Leo atafanya vizuri, kesho ataharibu) pengine ni kutoka na matumizi ya kinywaji kupita kiasi pamoja na kukosa muda wa kupumzika. Niliwahi kusema kuwa, kwa staili hii ya Banza Stone kushindwa kufuata miiko ya uimbaji, ni wazi kuwa atabakia kuwa mwanamuziki mzuri wa studio lakini akawa mwimbaji wa kubahatisha majukwaani. 
  Nini hasa kinachomfanya Banza ashindwe kutoa kazi mpya itakayotikisa kama enzi za “Elimu ya Mjina” na “Mtu Pesa”? kuna matatizo makubwa mawili – kudharau afya yake na kupuuzia kazi zake.
  Huwezi kutuliza akili na kutoa kazi bora kama afya yako haiko barabara, huwezi kutoa kazi nzuri kama huzingatii miiko ya kazi na kwa bahati mbaya au nzuri, Banza anawashauri wengi wazuri lakini usikivu sifuri. Binafsi kuna wakati nilijitahidi sana kumshauri Banza, ndugu zake wanajua hiyo kitu, pale nyumbani kwao Sinza huwa napokewa kama mtoto wa nyumbani na hata hivi ninavyoandika makala hii siandiki kwa kumchukia Banza bali ni kwaajili ya kumpenda.
  Banza Stone hajijali, Banza haogopi kuugua wala kufa. Nakumbuka wakati Amigolas amefariki nilikutana na Banza na nikamfahamisha juu ya kifo cha Amigo. Banza akanijibu hivi: “Mbona mimi sifi moja kwa moja? Nimeshakufa sijui mara ngapi, zaidi ya mara kumi lakini sifi kweli, kwanini?” alisema Banza huku akicheka kuashiria kuwa anatania, lakini mzaha huo unatoa tafsiri moja tu – haogopi kufa – na hilo linampelekea Banza kutojali afya yake hata kidogo.
  Banza hathamini kazi yake na ndiyo maana anaweza kupiga ‘mtindi’ kupitiliza bila kujali kuwa yupo kazini, hana muda kufanya promosheni, ni mara chache sana kumkisia Banza kwenye vyombo vya habari akifagilia kazi zake, Banza anapenda kuwa Mkurugenzi wakati anajua wazi kuwa yeye ni aina ya wasanii wanaotakiwa kuongozwa, hajajaaliwa kuwa kiongozi na ndio maana alishindwa kusimamisha bendi yake ya Bambino katika awamu mbili tofauti na pengine ni hali hiyo hiyo ndiyo inachangia bendi yao mpya (Wana Extra, baadae Rungwe Band) kutokuwa hai – katika umri wa miezi mitano ya bendi hiyo, imefanya jumla ya maonyesho yasiyozidi kumi.
  Pamoja na hayo Banza bado ana nafasi kubwa ya kuteka soko licha ya muziki wa dansi kufifia, Banza ni mmoja wa wanamuziki wachache wa muziki huu mwenye uwezo wa kupenya hadi kwenye himaya ya muziki wa kizazi kipya.
  Anachotakiwa kukifanya ni kubadika, soko bado linamhitaji Banza, ‘ufalme’ wake kwenye muziki wa dansi bado haujapokonywa, nyota yake ya kukubalika kuanzia kwa wagumu, masela, walala hoi hadi ‘ushuani’ kwa wenye nazo bado iko pale pale. BADILIKA BANZA.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: BADILIKA BANZA STONE SOKO BADO LINAKUHITAJI SANA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top