• HABARI MPYA

    Monday, January 26, 2015

    AZAM FC YAONDOKA KESHO ALFAJIRI KUWAFUATA TP MAZEMBE LUBUMBASHI

    Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
    KIKOSI cha wachezaji 24 pamoja na benchi la Ufundi na maofisa kadhaa wa klabu ya Azam FC kinatarajiwa kuondoka kesho Alfajiri Dar es Salaam kwenda Lubumbashi, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) kwa ajili ya kambi fupi ya wiki moja.
    Azam FC itakuwa Lubumbashi kwa kambi ya kujiandaa na mchezo wa Raundi ya Awali ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya El Merreikh ya Sudan mwezi ujao.
    Mtendaji Mkuu wa Azam FC, Saad Kawemba ameiambia BIN ZUBEIRY leo kwamba, kikiwa mjini humo, kikosi chao kitacheza mechi tatu za kirafiki ikiwemo dhidi ya wenyeji wao, TP Mazembe.
    Kikosi cha Azam FC kilichomenyana na Simba SC jana, kesho kinaenda Lubumbashi

    Mabingwa hao wa Tanzania Bara, Azam watacheza pia na Don Bosco ya Kinshasa na ZESCO United ya Zambia.
    Baada ya mechi ya Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara jana iliyoisha kwa sare ya 1-1 na Simba SC, wachezaji wa Azam FC walipewa mapumziko na wanatarajiwa kukutana jioni ya leo kwa ajili ya mazoezi mepesi tayari kwa safari ya Saa 11:00 Alfajiri kesho wakitumia ndege ya shirika la Kenya.
    Msafara huo utakaopitia Nairobi, Kenya unatarajiwa kutua Lubumbashi Saa 5:40 asubuhi na baada ya kambi hiyo, Azam FC itarejea Dar es Salaam Februari 4, tayari kabisa kwa mchezo wa kwanza na Merreikh Februari 15, Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam. Lakini kabla ya mchezo huo, Azam FC itacheza mbili za Ligi Kuu ikirejea Lubumbashi. 
    Kikosi cha Azam FC kinachotarajiwa kuondoka kesho ni makipa; Aishi Manula, Mwadini Ali, Jackson Wandwi na Khalid Mahadhi Hajji, mabeki Said Mourad, Gardiel Michael, David Mwantika, Shomary Kapombe, Erasto Nyoni, Aggrey Morris na Serge Wawa.
    Viungo ni Salum Abubakar ‘Sure Boy’, Kipre Balou, Mudathir Yahya, Frank Domayo, Brian Majwega, Amri Kiemba, Khamis Mcha ‘Vialli’, Kevin Friday na Himid Mao, wakati washambuliaji ni Didier Kavumbangu, John Bocco, Kipre Tchetche na Gaudence Mwaikimba. 
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: AZAM FC YAONDOKA KESHO ALFAJIRI KUWAFUATA TP MAZEMBE LUBUMBASHI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top