• HABARI MPYA

  Wednesday, January 28, 2015

  TUNA VIONGOZI WA OVYO MNO SIKU HIZI!

  ILIKUWA ni vigumu kuamini, lakini hicho ndicho kilichotokea. Wakati wauguzi na madaktari wanahangaika ili kuokoa maisha ya mchezaji Mganda, Emmanuel Okwi, jukwaani mashabiki walikuwa wanashangilia.
  Mashabiki wa Yanga walifurahi mchezaji yule alipogongwa na beki wa Azam FC, Aggrey Morris katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, timu hizo zikitoka 1-1 tena Okwi akitangulia kuifungia Simba.
  Niliwaelewa Yanga SC, hawampendi Okwi kwa sababu kubwa alikuwa mchezaji wao na akaondoka kurejea Simba SC akiwa bado ana Mkataba na klabu yao.

  Okwi alipata nguvu ya kisheria kuondoka klabu hiyo, baada ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kupitia Kamati ya Sheria Maadili na Hadhi za Wachezaji kujiridhisha Yanga SC ilikiuka vipengele vya Mkataba huo.   
  Ile iliwauma Yanga SC na wakawa hawamtakii mema tena Okwi, ila sikuwahi kufikiria kwamba ni kwa kiwango hata cha kumuombea afe. Haikuwahi kuniingia akilini. Nilikuwa tu najua, Okwi hakatizi salama kwenye msitu wa mashabiki wa Yanga. 
  Mapigo ya moyo wa Okwi yalisimama baada ya kupigwa kiwiko na Aggrey Morris katika pilika za mchezo huo na ikabidi akimbizwe hospitali ya Rufaa ya Muhimbili, ambako alitibiwa na kurejea katika hali ya kawaida. 
  Daktari wa Simba SC, Yassin Gembe alisema baadaye Jumapili kwamba mshambuliaji huyo ametoka salama hospitali, lakini amechungulia kifo.
  Gembe alisema kwamba Okwi amerejea nyumbani baada ya matibabu katika hospitali ya Muhimbili, lakini alikumbana na mkasa mbaya maishani.
  “Okwi aligongwa kiwiko nyuma ya kichwa kwenye mishipa ya fahamu, kwa hiyo akapoteza fahamu uwanjani. Ilikuwa mbaya sana, angeweza kupoteza maisha, lakini hali ile tuliidhibiti wakati tunampa huduma ya kwanza uwanjani,”.
  “Baada ya hapo, tukaingia naye ndani kwenye zahanati ndogo ya Uwanja, kuendelea kumpa tiba hadi fahamu zikamrejea, lakini hali yake haikuwa nzuri sana, ikabidi tumkimbize Muhimbili, ambako baada ya tiba ya takriban saa mbili, sasa yuko vizuri,”alisema Gembe.
  Okwi alianza mazoezi mepesi jana, baada ya mapumziko ya kutwa nzima ya juzi, ingawa hataweza kucheza leo Simba SC ikimenyana na Mbeya City Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
  Wakati nazungumza na Dk Gembe, na nilipokumbuka namna ambavyo mashabiki wa Yanga SC walivyokuwa wakishangilia, nilisikitika mno. Nilisikitika kwa sababu tumefikia katika hatua mbaya.
  Kwamba mtu anaweza akafa sisi tunashangilia. Sijui dunia itatuona ni watu wa ajabu kiasi gani. Lakini ni kipi kimetufikisha huku? Viongozi mashabiki, ndiyo tatizo kuu la soka yetu kwa sasa.
  Lazima kuwe na tofauti kubwa kati ya kiongozi na shabiki, lakini kwa sasa katika soka ya Tanzania, viongozi ndiyo mashabiki kuliko mashabiki wenyewe. Tatizo.
  Wanashabikia ujinga. Wanashabikia upumbavu. Wanawaongoza vibaya wapenzi wa timu zao, ndiyo maana wanafikia hadi kung’oa viti viwanjani. 
  Wanawaongoza vibaya wachezaji wao, ndiyo maana wengi wao nidhamu yao ni mbovu. Viongozi wa aina hii ni hatari sana kwa soka yetu- sasa wanatufikisha kwamba wapenzi wapo uwanjani wanashangilia mchezaji anayepambana na uhai wake kuepuka kifo.
  Miaka ya nyuma kidogo, hadi ya 1990, mchezaji akianguka kwa pigo ambalo watu wanajiridhisha ni la hatari, Uwanja wote unakuwa kimya, kila mtu akifanya ibada na sala yake kumuombea.
  Wale wapenzi wa mpira wa wakati ule walikuwa binadamu haswaa, ila sisi wa siku hizi ni binadamu wa aina gani? Tatizo viongozi. Vongozi wetu wengi ni ‘vilaza’, hawajitambui na ndiyo maana sasa hata Ligi Kuu inakuwa kama mashindano ya mchangani, uhuni ‘undava’ vimekithiri.
  Mchezaji anamfanyia mwenzake mambo yasiyo ya kiungwana, kiongozi anazungumza hadharani, eti soka siyo kuuza nyanya na Shirikisho la Soka la nchi linamuacha hivi hivi huyu mtu. 
  Hizi ni kauli za uchochezi zisizotakiwa kabisa kama tunataka kutengeneza mpira wenye adabu na wa kiungwana kama ilivyo kaulimbiu ya wenye mpira wao, FIFA. 
  Kwa kweli wakati huu, tuna viongozi wa ovyo sana na kama Rais wa TFF, Jamal Malinzi hatasimama imara kupambana juu ya maadili ya kiuongozi, basi hali itakuwa mbaya zaidi.
  Rais aliyemaliza muda wake TFF, Leodegar Tenga, kama kuna mambo ambayo yatamfanya akumbukwe muda mrefu, ni kuweza kutengeneza taasisi rasmi ya mpira.
  Tenga alipambana sana na maadili na watu walinyooka kwa kiasi kikubwa. Lakini leo viongozi wanazungumza ufedhuli, wanaachwa tu. Yule kiongozi wa Ruvu aliyesema soka siyo kuuza nyanya ni wa kufungia, ili liwe fundisho kwa wengine.
  Msemaji wa Yanga SC, Jerry Muro alimfuata mshika kibendera uwanjani Jumamosi, timu yake ikicheza na Polisi kumlalamikia amewakatalia bao. Hasira za Muro ziliishia kwenye kulalamika tu, lakini je zingemtuma kumchapa makofi yule mwamuzi?
  Malinzi kama anataka wepesi wa kuongoza soka ya nchi hii, kwanza ahakikishe anawanyoosha viongozi. Tuna viongozi wa ovyo mno siku hizi katika soka yetu! 
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: TUNA VIONGOZI WA OVYO MNO SIKU HIZI! Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top