• HABARI MPYA

  Jumamosi, Januari 31, 2015

  SIMBA SC KATIKA MTIHANI MZITO LEO

  Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
  LIGI Kuu ya Vodacom Tanzania Bara inatarajiwa kuendelea leo, huku vigogo Simba SC wakiwa wenyeji wa JKT Ruvu Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
  Ikitoka kupoteza mchezo mbele ya Mbeya City katikati ya wiki, Simba SC itakuwa na mtihani mwingine leo mbele ya timu ya Jeshi la Kujenga Taifa, inayofundishwa na Freddy Felix Minziro, beki na kocha wa zamani wa mahasimu wao, Yanga SC.
  Beki Hassan Kessy aliyekosekana katika mchezo uliopita kwa sababu ya kadi za njano, leo anatarajiwa kurejea kikosini sambamba na mshambuliaji, Emmanuel Okwi aliyekuwa majeruhi.
  Kikosi cha Simba SC kilichofungwa 2-1 na Mbeya City Jumatano

  Kiungo Said Ndemla ataendelea kukosekana kwenye kikosi cha Mserbia Goran Kopunovic akiwa anauguza nyama za paja na Daktari wa Simba SC, Yassin Gembe amesema Ibrahim Hajibu yuko fiti.
  Mshambuliaji huyo anayeinukia vizuri katika kikosi cha Wekundu wa Msimbazi, alitolewa kipindi cha pili katika mechi na Mbeya City akiwa anachechemea baada ya kuumia.
  Lakini Gembe amesema hayakuwa maumivu makubwa na mchezaji huyo zao la kikosi cha vijana cha Simba SC amefanya mazoezi awamu zote zote baada ya hapo.
  Kuna uwezekano Kopunovic akamrudisha langoni kipa mkongwe Ivo Mapunda, baada ya chipukizi Peter Manyika kuruhusu mabao matatu katika mechi mbili zilizopita za Ligi, moja la penalti.
  Kipigo cha Mbeya City kimeonekana kuivuruga Simba SC, viongozi wakilumbana na kutupiana lawama kwa sababu mbalimbali, ikiwemo ukiukwaji wa maadili ya kiuongozi.
  Kocha Msaidizi, Suleiman Matola ameripotiwa kuomba kupunguziwa majukumu na Rais Evans Aveva amesema uongozi unalitafakari hilo. 
  Kwa kiasi fulani hamkani si shwari ndani ya Simba SC na ni ushindi pekee katika mchezo wa leo, ambao utarejesha amani Msimbazi, kwani hata kocha Mkuu, Kopunovic anaonekana kuanza ‘kuvurugwa’ na hali halisi inayoendelea.
  Mserbia huyo alianza vizuri kazi Msimbazi baada ya kurithi mikoba ya Mzambia, Patrick Phiri Januari akiiwezesha timu kushinda mechi sita mfululizo bila kuruhusu bao, ikiwemo kutwaa Kombe la Mapinduzi visiwani Zanzibar. 
  Lakini baada ya sare ya 1-1 katika mchezo wa saba na Azam FC, akapoteza mchezo uliofuata na Mbeya City 2-1.
  Mechi nyingine za Ligi Kuu leo ni kati ya Coastal Union na Mtibwa Sugar Uwanja wa Mkwakwani, Tanga, Ruvu Shooting na Stand United Uwanja wa Mabatini, Mlandizi, Pwani, Prisons na Kagera Sugar Uwanja wa Sokoine Mbeya, Polisi Moro na 
  Mbeya City Uwanja wa Jamhuri, Morogoro, wakati kesho Yanga SC watakuwa wenyeji wa Ndanda FC ya Mtwara Uwanja wa Taifa.
  Mchezo kati ya Mgambo JKT na mabingwa watetezi, Azam FC uliokuwa ufanyike leo, umeahirishwa. Azam FC wako ziarani Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: SIMBA SC KATIKA MTIHANI MZITO LEO Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top