• HABARI MPYA

  Friday, January 21, 2022

  ALGERIA YAVULIWA UBINGWA AFCON, TUNISIA YAPENYA MLANGO WA DHARULA


  RASMI, Algeria jana wamevuliwa ubingwa baada ya kuchapwa 3-1 na Ivory Coast katika mchezo wa mwisho wa Kundi E Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika usiku wa Alhamisi Uwanja wa Douala nchini Cameroon.
  Mabao ya Tembo wa Ivory Coast yamefungwa na Franck Kessie dakika ya 22, Ibrahim Sangare dakika ya 39 na Nicolas Pepe dakika ya 54, wakati la Algeria waliotwaa taji hilo mwaka 2019 nchini Misri limefungwa na Sofiane Bendebka dakika ya 73, kufuatia Riyad Mahrez kukosa penalti dakika ya 60.
  Mechi nyingine ya Kundi E, bao pekee la Pablo Ganet dakika ya 38 limeipa Equatorial Guinea ushindi wa 1-0 dhidi ya Sierra Leone Uwanja wa Limbe.
  Ivory Coast inamaliza na pointi saba kileleni, ikifuatiwa na Equatorial Guinea pointi sita na zote Sina kwenda 16 Bora, wakati Sierra Leone iliyomaliza na pointi mbili na Algeria pointi moja safari inaishia hapa.
  Na mechi za Kundi F, vigogo wengine barani, Tunisia wametupwa nje baada ya kuchapwa 1-0 na Gambia bao pekee la Abdoulie Jallow dakika ya  90 Uwanja wa Limbe.
  Nayo Mali ikaichapa Mauritania 2-0, mabao ya Massadio Haïdara dakika ya pili na Ibrahima Koné kwa penalti dakika y 49 Uwanja wa Douala.
  Mali imemaliza na pointi saba, sawa na Gambia na zote zinakwenda 16 Bora, wakati Tunisia  inafuzu kama mmoja wa washindi wa tatu bora kwa kumaliza na pointi tatu na Mauritania iliyomaliza mikono mitupu inaaga mashindano.
  Hatua ya 16 Bora itaanza Jumapili kwa Burkina Faso kumenyana na Gabon, Nigeria na Tunisia, Jumatatu ni Guinea na Gambia na Cameroon dhidi ya Comoro.
  Januari 25 ni Senegal na Cape Verde na Morocco dhidi ya Malawi, wakati Hatua hiyo ya 16 itakamilishwa Januari 26 kwa mechi mbili kali tupu; Ivory Coast na Misri na Mali dhidi ya Equatorial Guinea.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: ALGERIA YAVULIWA UBINGWA AFCON, TUNISIA YAPENYA MLANGO WA DHARULA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top