• HABARI MPYA

  Sunday, January 16, 2022

  YANGA YAIZIMA COASTAL MKWAKWANI,YAIPIGA 2-0

  VIGOGO, Yanga SC wamerejea na moto wao kwenye Ligi Kuu ya Tanzania Bara baada ya ushindi wa 2-0 dhidi ya wenyeji, Coastal Union jioni ya leo Uwanja wa Mkwakwani Jijini Tanga.
  Mabao ya Yanga SC leo yamefungwa na mshambuliaji, Fiston Kalala Mayele dakika ya 41 kwa kichwa akimalizia krosi ya Mkongo mwenzake waliyetoka naye AS Vita ya kwao, Kinshasa msimu huu, beki Djuma Shabani na kiungo Mrundi, Saido Ntibanzokiza dakika ya 90 akimalizia pasi ya winga mzawa, Farid Mussa Malik.
  Kwa ushindi huo, Yanga SC inayofundishwa na kocha Mtunisia Mohamed Nasreddine Nabi inafikisha pointi 32 baada ya kucheza mechi 12 na kuendelea kuongoza ligi kwa pointi nane zaidi ya mabingwa watetezi, Simba SC ambao hata hivyo wana mechi mbili mkononi.
  Coastal Union inayofundishwa na kocha Mmarekani, Melis Medo inabaki na pointi zake 17 za mechi 12 pia katika nafasi ya nne.
  Mechi nyingine ya Ligi Kuu leo, wenyeji Tanzania Prisons wamechapwa 2-0 nyumbani na KMC, mabao ya Kelvin Kijiri dakika ya 21 na Ally Ramadhani dakika ya 88 Uwanja wa Nelson Mandela, Sumbawanga mkoani Rukwa.
  KMC inafikisha pointi 14 katika nafasi ya nane na Tanzania Prisons inabaki na pointi zake 11 katika nafasi ya 13 baada ya timu zote kucheza mechi 12.


  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: YANGA YAIZIMA COASTAL MKWAKWANI,YAIPIGA 2-0 Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top