• HABARI MPYA

  Saturday, January 15, 2022

  MOROCCO YASONGA MBELE AFCON, SENEGAL YASHIKWA


  TIMU ya taifa ya Morocco imeendeleza wimbi la ushindi katika Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika baada ya kuichapa Comoro mabao 2-0 usiku wa Ijumaa katika mchezo wa Kundi C Uwanja wa Ahmadou Ahidjo Jijini Yaoundé.
  Mabao ya Morocco yamefungwa na kiungo wa Standard Liège ya Ubelgiji, Selim Amallah dakika ya 16 na mshambuliaji wa 
  Alkmaar Zaanstreek ya Uholanzi, Zakaria Aboukhlal dakika ya 89 na kwa ushindi huo, Simba wa Atlasi wanafikisha pointi sita na kufuzu Hatua ya mtoano ya michuano hiyo mbele ya Gabon yenye pointi nne, Ghana moja na Comoro ambayo haina pointi.
  Mechi nyingine ya Kundi C jana, Gabon ilitoa sare ya 1 -1 na Ghana hapo hapo Ahmadou Ahidjo, Yaoundé.
  Ghana ilitangulia kwa bao la mshambuliaji wa Al Sadd ya Qatar, André Ayew dakika ya 18, kabla ya mshambuliaji wa Marmande ya Ufaransa, Jim Émilien Ngowet Allevinah kuisawazishia Gabon dakika ya 88.
  Mechi za Kundi B, Senegal ililazimishwa sare ya 0-0 na 
  Guinea na Malawi ikailaza Zimbabwe 2-1 Uwanja wa Bafoussam.
  Mabao yote yalifungwa na nyota wa klabu za ya Afrika Kusini kwenye mechi hiyo, Zimbabwe ilitangulia kwa bao la kiungo wa JDR Stars, Ishmael Wadi dakika ya 38, kabla ya mshambuliaji wa Orlando Pirates, Hellings Frank Mhango kuifungia mawili Malawi dakika ya 43 na 58.
  Sasa Guinea na Senegal zote zina pointi nne kila moja, zikifuatiwa na Malawi pointi tatu na Zimbabwe inashika mkia haina pointi.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: MOROCCO YASONGA MBELE AFCON, SENEGAL YASHIKWA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top