• HABARI MPYA

    Thursday, October 15, 2020

    MWAKINYO KUWANIA UBINGWA WA MABARA DHIDI YA MUARGENTINA

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    BINGWA wa mabara wa ngumi za kulipwa uzito wa Super Welter, Hassan Mwakinyo atautetea mkanda wake wa Chama cha WBF Novemba 13 dhidi ya bondia wa Argentina Jose Carlos Paz.
    Pambano hayo yamepewa jina  la  Dar Fight Night yameandaliwa na kampuni ya Jackson Group Sports.
    Mbali ya kutetea mkanda huo, Mwakinyo pia atawania ubingwa wa mabara  wa uzito huo huo wa Chama cha IBA. Pambano hilo limepangwa kufanyika kwenye ukumbj wa Next Door Arena.
    Mkurugenzi wa The Jackson Group Sports Kelvin Twissa amesema siku hiyo mabondia kutoka nchi tano watazichapa kumsindikiza Mwakinyo na Paz, akiwamo aliyekuwa bingwa wa dunia wa WBC, Fatuma Zarika kutoka Kenya.

    Mkurugenzi wa kampuni ya Jackson Group Sports Kelvin Twisa (wa pili kulia) akiutambulisha mkanda wa mabara wa WBF ambao bondia Hassan Mwakinyo (wa pili kulia) atautetea dhidi ya bondia Jose Carlos Paz Novemba 13 kwenye ukumbi wa Next Door Arena, Masaki. Wa kwanza kulia ni bonda Dulla Mbabe na wa kwanza kushoto ni bondia Zulfa Macho

    Twisa alisema kuwa  Zarika atazichapa na Patience Mastara wa  Zimbabwe, na Zulfa Yusuph Macho atacheza na Alice Mbewe wa Zimbabwe.
    Pia siku hiyo, bondia Abdallah Pazi maarufu kwa jina la Dullah Mbabe  atacheza na Alex Kabangu wa DR Congo.
    Alisema kuwa wameamua kuingia kwenye mchezo wa ngumi kutokana na kutambua vipaji vya mabondia mbalimbali hasa Mwakinyo ambaye anafanya vizuri katika mapambano yake.
    "Siku hiyo kutakuwa na pambano  makubwa ambapo mabondia kutoka nchi sita, Argentina, DR Congo, Kenya, Uganda, Zimbabwe na wenyeji Tanzania watapigana, ni siku ambayo mashabiki wa ngumi za kulipwa wataona kitu tofauti kabisa katika mchezo huo, " alisema Twisa.
    Alisema kuwa kampuni yao chini ya udhamini wa Azam TV na Asas  ina uzoefu mkubwa katika kuandaa matamasha, masoko na shughuli mbalimbali na kuahidi kufanya jambo la kihistoria hapa nchini.
    "Tunataka kuona mabondia wanaendelea kwa kupata mapambano mengi ya ngumi na kinacho endana na kazi yao, tulifanya kazi na Mwakinyo kwa miaka mitatu na kuona ufanisi wake, tumeamua kuendelea naye na mabondia wengine wa Tanzania, tutaubadili mchezo wa ngumi nchini," alisema.
    Kwa upande wake, Mwakinyo alisema kuwa hiyo ni fursa kwake na kuahidi kufanya vyema siku hiyo.
    "Namshukuru Twisa na kampuni ya Jackson Group Sports ambao wameonyesha nia ya kuubadili mchezo wa ngumi za kulipwa, sitawaangusha watanzania," alisema Mwakinyo.
    Mwakilishi wa WBF nchini Tanzania,  Chatta Michael alisema kuwa rais wa shirikisho hilo, Goldberg Howard atasimamia mapambano hayo.

    Mkurugenzi wa kampuni ya Jackson Group Sports Kelvin Twisa (katikati) akizungumza wakati wa utambulisho wa mapambano ya Dar Fight Night yaliyopangwa kufanyika Novemba 13 kwenye ukumbi wa Next Door Arena kati ya bondia Hassan Mwakinyo (wa pili kulia) dhidi ya bondia Jose Carlos Paz wa Argentina. Wa kwanza kulia ni bonda Dulla Mbabe  na wa kwanza kushoto ni bondia Zulfa Macho na pili kushoto ni mwakilishi wa WBF Tanzania, Chatta Michael.

    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: MWAKINYO KUWANIA UBINGWA WA MABARA DHIDI YA MUARGENTINA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top