• HABARI MPYA

    Sunday, October 04, 2020

    KRMPOTIC AENDELEZA REKODI YA KUTODUMU KWENYE TIMU, AFUKUZWA NA YANGA BAADA MWEZI TU

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    KLABU ya Yanga imemfuta kazi kocha Mserbia, Zlatko Krmpotic mwezi mmoja tu tangu aajiriwe  kuchukua nafasi ya Mbelgiji, Luc Eymael aliyefukuzwa pia Agosti mwaka huu.
    Taarifa iliyotolewa na Yanga SC baada ya mchezo wake wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara ikishinda 3-0 dhidi ya Coastal Union Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam – imesema kwamba wameamua kuachana na Mserbia huyo baada ya maridhiano ya pande zote mbili.
    Yanga SC sasa itakuwa chini ya aliyekuwa Kocha Msaidizi, Juma Mwambusi na aliyekuwa kocha wa timu ya vijana, Said Maulid ‘SMG’ kuelekea mchezo dhidi ya mahasimu wao wa jadi, Simba SC Oktoba 18, Uwanja wa Mkapa.

    Krmpotic anayeendeleza rekodi yake ya kutodumu kwenye timu, anaondolewa Yanga SC baada ya mechi nane tu, zikiwemo tano za Ligi Kuu, tatu za kirafiki akishinda saba na droo moja – ingawa anaiacha timu inaongoza ligi ya Tanzania Bara. 
    Baada ya ushindi wa 3-0 dhidi ya Coastal Union, Yanga SC inafikisha pointi 13 katika mchezo wa tano, sasa ikiongoza Ligi Kuu kwa pointi tatu zaidi ya mabingwa watetezi, Simba SC ambao wana mechi moja mkononi na Jumapili watakuwa wageni wa JKT Tanzania Uwanja wa Jamhuri. 
    Kabla ya kutua Yanga, Krmpotic mwenye umri wa miaka 62, mzaliwa wa Belgrade, alianzia kwenye kucheza soka katika nafasi ya ulinzi Red Star Belgrade ya kwao kwa misimu tisa, na kushinda mataji matano kati ya mwaka 1977 na 1986, akichezea mechi zaidi ya 200 za mashindano yote. 
    Baada ya hapo akaenda Uturuki na kuchezea kwa misimu miwili klabu ya Genclerbirligi kati ya 1986 na 1988 kabla ya kurejea nyumbani kwao kumalizia soka yake katika klabu ya AIK Backa Topola.
    Krmpotic pia aliichezea timu ya taifa ya ya Yugoslavia mechi mbili katika fainali za Kombe la Duna mwaka 1982, timu hiyo ikimaliza kwenye nafasi ya tatu katika Kundi la Tano. 
    Awali, Krmpotic alishinda Kombe la Matafa ya Ulaya kwa vijana chini ya umri wa miaka 21 ‘UEFA Euro U-21’ mwaka 1978 akiwa na Yugoslavia.
    Na tangu awe kocha, Krmpotić amefundisha klabu tofauti katika nchi 12 duniani, ambazo ni AIK Bačka Topola, OFK Beograd za Serbia, Degerfors IF ya Sweden, Sloga Jugomagnat ya FYR Macedonia, Ankaragücü ya Uturuki, Paniliakos ya Ugiriki, Nea Salamis ya Cyprus, Kairat ya Kazakhstan na Kazma ya Kuwait.
    Nyingine ni Don Bosco ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), ZESCO United ya Zambia, Jwaneng Galaxy ya Botswana, APR ya Rwanda, Polokwane City na Royal Eagles za Afrika Kusini.
    Pia aliziongoza timu za taifa za vijana za Serbia na Montenegro chini ya umri wa miaka 17 mwaka 2005 na U19 ya Serbia 2007 na 2008.
    Krmpotic mwenye uraia wa Croatia amewahi kushinda tuzo za Kocha Bora wa DRC msimu wa 2016-2017, Kocha Bora wa Ligi Kuu ya Zambia msimu wa 2017-2018, Kocha Bora wa Ligi Kuu ya Botswana mwaka 2018 na Kocha Bora wa Afrika 2017-2018.
    Ujio wake Jangwani ulifuatia mpango wa Yanga kumchukua Mrundi, Cedric Kaze aliyekuwa anafundisha akademi za Barcelona nchini Canada kushindikana kufuatia kuachana na kocha Mbelgiji, Luc Eymael aliyedumu kwa miezi saba tangu Januari.
    REKODI YA MSERBIA ZLATKO KRMPOTIC YANGA SC
    1. Yanga SC 2-0 Aigle Noir/Burundi (Wiki ya Mwananchi Mkapa)
    2. Yanga SC 1-1 Tanzania Prisons (Ligi Kuu Mkapa)
    3. Yanga SC 1-0 Mbeya City (Ligi Kuu Mkapa)
    4. Yanga SC 2-0 Mlandege SC (Kirafiki Chamazi)
    5. Yanga SC 1-0 Kagera Sugar (Ligi Kuu Kaitaba)
    6. Yanga SC 1-0 Mtibwa Sugar (Ligi Kuu Jamhuri)
    7. Yanga SC 2-0 KMKM (Kirafiki Chamazi)
    8. Yanga SC 3-0 Coastal Union (Ligi Kuu Mkapa)
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: KRMPOTIC AENDELEZA REKODI YA KUTODUMU KWENYE TIMU, AFUKUZWA NA YANGA BAADA MWEZI TU Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top