• HABARI MPYA

  Jumamosi, Oktoba 03, 2020

  YANGA SC YAPANDA KILELENI LIGI KUU TANZANIA BARA BAADA YA KUICHAPA COASTAL UNION 3-0

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  VIGOGO, Yanga SC wamepanda kileleni mwa Ligi Kuu ya Tanzania Bara baada ya ushindi wa 3-0 dhidi ya Coastal Union Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.
  Yanga SC inafikisha pointi 13 baada ya ushindi huo katika mchezo wa tano, sasa ikiongoza Ligi Kuu kwa pointi tatu dhidi ya mabingwa watetezi, Simba SC ambao wana mechi moja mkononi. 
  Dakika 45 za mchezo huo uliochezeshwa na refa Suleiman Nonga wa Arusha, aliyesaidiwa na Charles Simon na Sunday Komba pembezoni mwa Uwanja zlmalzka bla nyavu kuguswa.
  Na kipindi cha pili ndipo mambo yalipowanyookea wana Jangwani kwa kufanikiwa kupata mabao yao yote matatu na yote yakifungwa na wachezaji wa kigeni.

  Alianza kiungo Muangola, Carlos Carlinhos dakika ya tatu tu kipindi cha pili kufunga bao la kwanza kwa kichwa akimalizia krosi ya kiungo Deus Kaseke aliyechukua nafasi ya beki wa kulia, Kibwana Shomari. 
  Akafuatia Mnyarwanda Haruna Niyonzima kufunga kwa shuti kali kutoka pembeni kushoto dakika ya 52 akimalizia krosi ya winga Mkongo, Tuisila Kisinda kutoka kulia. 
  Mshambuliaji kutoka Burkina Faso, Yacouba Sogne akafungua akaunti yake ya mabao Jangwani kwa kufunga bao zuri dakika ya 63 akimpiga chenga kipa Abubakar Ibrahim baada ya kuwekewa pasi na Mchezaji Bora wa Yanga mwezi Septemba, kiungo Mkongo Tonombe Mukoko.
  Mechi zilizotangulia leo, Mwadui FC imepata ushindi wa ugenini wa 1-0 dhidi ya Namungo FC Uwanja wa Majaliwa, Ruangwa mkoani Lindi, bao pekee la Ismail Ally dakika ya saba.
  Mbeya City wamelazimishwa sare ya bila kufungana na ndugu zao, Tanzania Prisons Uwanja wa Sokoine Jijini Mbeya na Gwambina FC imeichapa Ihefu FC 2-0, mabao ya Meshack Abraham dakika ya 33 na 48 Uwanja wa CCM Kirumba Jijini Mwanza.
  Ligi Kuu itaendelea kesho kwa mechi tatu; Biashara United na Mtibwa Sugar Uwanja wa Karume mjini Musoma mkoani Mara Saa 8:00 mchana, JKT Tanzania na Simba SC Uwanja wa Jamhuri Jijini Dodoma Saa 10:00 jioni na Azam FC na Kagera Sugar Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam Saa 1:00 usiku.
  Raundi ya tano itahitimishwa keshokutwa kwa mchezo mmoja, kati ya KMC na Polisi Tanzania Uwanja wa Uhuru Jijini Dar es Salaam.
  Mara tu baada ya mchezo huo, Yanga ikatangaza kuachana na kocha Mserbia, Zlatko Krmpotic mwezi mmoja tu tangu aajiriwe  kuchukua nafasi ya Mbelgiji, Luc Eymael aliyefukuzwa pia Agosti mwaka huu.
  Kikosi cha Yanga SC kilikuwa; Metacha Mnata, Kibwana Shomari/Deus Kaseke dk46, Adeyoum Ahmed, Lamine Moro, Bakari Mwamnyeto, Feisal Salum, Zawadi Mauya/Haruna Niyonzima dk46, Mukoko Tonombe, Yacouba Sogne, Carlos Carlinhos na Tuisila Kisinda/Ditram Nchimbi dk85.
  Coastal Union; Abubakar Ibrahim, Hassan Kibailo, Hance Masoud, Seif Bihaki/Rashid Chambo dk46, Peter Mwangosi/Muhsin Malima dk72, Salum Ally, Abdul Suleiman/Radhin Hafidh dk46, Mtenje Albano, Mudathir Said, Issa Abushehe na Hamad Majimengi.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: YANGA SC YAPANDA KILELENI LIGI KUU TANZANIA BARA BAADA YA KUICHAPA COASTAL UNION 3-0 Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top