• HABARI MPYA

  Ijumaa, Oktoba 30, 2020

  SURE BOY AINUSURU AZAM FC KUFUNGWA NYUMBANI, YATOA SARE 1-1 NA JKT TANZANIA CHAMAZI

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  WENYEJI, Azam FC wamelazimishwa sare ya kufungana bao 1-1 na JKT Tanzania katika mchezo wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara usiku wa leo Uwanja wa Azam Complex, Chamazi nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam. 
  Pamoja na sare hiyo, Azam FC inaendelea kuongoza Ligi Kuu kwa pointi zake 22 baada ya kucheza mechi tisa sasa, ikiwazidi pointi tatu mabingwa wa kihistoria, Yanga SC ambao hata hivyo wana mechi mbili mkononi.
  Katika mchezo wa leo, Michael Aidan Pius alianza kuifungia JKT Tanzania dakika ya 43, kabla ya Nahodha na kiungo hodari, Salum Abubakar ‘Sure Boy’ kuisawazishia Azam FC dakika ya 78.

  Baada ya mwanzo mzuri ikishinda mechi saba mfululizo, Azam FC ilipunguzwa kasi wiki iliyopita kwa kuchapwa 1-0 na Mtibwa Sugar Uwanja wa CCM Gairo, Morogoro na leo imetoa sare nyumbani. 
  Mechi nyingine ya Ligi Kuu leo, KMC imeibuka na ushindi wa 3-0 dhidi ya wenyeji, Gwambina FC Uwanja wa Gwambina, Misungwi mkoani Mwanza, mabao ya Lusajo Mwaikenda dakika ya 43, Relliants Lusajo dakika ya 87 na David Bryson dakika ya 90 na ushei.
  Ligi Kuu itaendelea kesho kwa mechi nne, mabingwa watetezi, Simba SC wakiwa wenyeji wa Mwadui FC Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam, Tanzania Prisons na Polisi Tanzania Uwanja wa Mandela, Sumbawanga mkoani Rumwa, Namungo FC na Dodoma Jiji Uwanja wa Majaliwa, Ruangwa mkoani Lindi na Biashara United dhidi ya Yanga SC Uwanja wa Karume, Musoma mkoani Mara.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: SURE BOY AINUSURU AZAM FC KUFUNGWA NYUMBANI, YATOA SARE 1-1 NA JKT TANZANIA CHAMAZI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top