• HABARI MPYA

  Saturday, October 31, 2020

  SIMBA SC WAZINDUKA KUTOKA KWENYE VIPIGO VIWILI MFULULIZO NA KUITANDIKA MWADUI FC 5-0

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  MABINGWA watetezi, Simba SC wamezinduka kutoka kwenye vipigo viwili mfululizo baada ya kuichapa Mwadui FC mabao 5-0 jioni ya leo Uwanja wa Uhuru Jijini Dar es Salaam.
  Ushindi huo wa kwanza katika mechi tatu, unaifanya Simba SC inayofundishwa na kocha Mbelgiji, Sven Ludwig Vandenbroeck ifikishe pointi 16 baada ya kucheza mechi nane na kurejea nafasi ya tatu kwenye msimamo wa Ligi Kuu nyuma ya Azam FC na Yanga wenye pointi 22 kila mmoja.
  Nahodha na mshambuliaji, John Raphael Bocco leo amefunga mabao mawili katika ushindi huo, la kwanza dakika ya 25 akimalizia pasi ya kiungi Mzambia, Clatous Chama na la pili dakika ya 64 akimalizia kazi nzuri ya mtokea benchi Hassan Dilunga.


  Kiungo wa zamani wa Yanga SCm, Dilunga naye akafunga mabao mawili, la tatu dakika 81 akimalizia pasi ya mtokea benchi mwenzake, Ibrahim Ajibu na la nne dakika ya 86 akimalizia pasi ya Said Ndemla.
  Ndemla ambaye amerejea kwenye kikosi cha kwanza cha Simba SC msimu huu baada ya kusota benchi kwa muda mrefu msimu uliopita – akakamilisha shangwe za mabao kwa Wekundu wa Msimbazi baadaya kufunga bao la tano dakika ya 90.
  Ushindi huo ni ahueni kwa mabingwa hao wa watetezi, kufuatia kupoteza mechi mbili mfululizo zilizopita zote wakichapwa 1-0 na Tanzania Prisons huko Sumbawanga mkoani Rukwa na Ruvu Shooting hapa Dar es Salaam.
  Kikosi cha Simba SC leo kilikuwa; Beno Kakolanya, Shomari Kapombe, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’, Joash Oyango, Pascal Wawa, Jonas Mkude, Rally Bwalya/Hassan Dilunga dk60, Said Ndemla, John Bocco/Ibrahim Ajibu dk70, Clatous Chama/ Fransis Kahata dk85 na Luis Miquissone.
  Mwadui FC; Mussa Mbisa, Jackson Shiga/Lilan Hussein dk67, Shaaban Kingazi, Halfan Mbarouk, Joram Mgeveke, Abbas Kapombe, Abubakar Kambi, Enrick Nkosi, Deogratius Anthony, Ismail Ally na Herman Masenga/Msenda Amri dk77.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: SIMBA SC WAZINDUKA KUTOKA KWENYE VIPIGO VIWILI MFULULIZO NA KUITANDIKA MWADUI FC 5-0 Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top