• HABARI MPYA

    Monday, April 13, 2015

    ALLY CHOCKY BILA BANZA STONE SAWA NA RAY BILA KANUMBA

    NILIWAHI kuandika wiki kadhaa zilizopita kuwa Asha Baraka na Ally Chocky wanahitajiana sana na kwa bahati nzuri leo hii watu hao wawili wamekutana tena na sasa wanafanya kazi pamoja.
    Kwa faida ya ambao hawakubahatika kusoma makala hiyo ya Chocky na Asha Baraka, naomba nirudie japo aya tatu kati ya 15 nilizokuwa nimeandika.
    Niliandika hivi: “Twanga Pepeta imeyumba, imekosa tungo zenye mashiko,  Twanga Pepeta inakosa nidhamu ya kutosha miongoni mwa wasanii ndani na nje ya jukwaa, Twanga Pepeta bado haijampata mrithi wa marehmu Abuu Semhando aliyekuwa mkali kama pilipili pale linapokuja suala la uwajibikaji. 
    Kwa sasa simuoni mwingine anayeweza kuyafunika yote hayo zaidi ya Ally Chocky na ndio maana nikasema kuwa kama kuna kipindi ambacho Asha Baraka anamhitaji Ally Chocky basi ni sasa kuliko kipindi chochote kile huko nyuma.
    “Lakini pia niseme yafuatayo kwa Chocky: Biashara ya muziki wa dansi imekuwa ngumu, Extra Bongo inapata wakati mgumu kupenya kwenye soko hili gumu, gharama za uendeshaji bendi ni kubwa kuliko kinachoingia, licha ya kuwa uwezo wake bado ni mkubwa sana lakini mvuto wake wa kimuziki umepungua na unahitaji ‘kubustiwa’ – sehemu pekee inayomfaa kwa wakati huu ni Twanga Pepeta. 
    “Sisemi kuwa Twanga Pepeta bila Chocky haiwezekani wala sisemi kuwa Chocky bila Twanga Pepeta haiwezekani, la hasha! ila nasema tu kuwa Asha Baraka na Chocky mnahitajiana sana kwa sasa lakini ni ujeuri wenu, najua mkiweka kando jeuri zenu (kama bado hamjaweka) basi tutashuhudia kitu kimoja kitakachopasua anga za muziki wa dansi”. Hayo ni baadhi ya mambo niliyoyaandika.
    Chocky amerejea Twanga na hivi sasa yuko chimbo akijiandaa kupakua nyimbo tatu mpya “Kichwa Chini”, “Usiyaogope Maisha” na “No Discussion”.
    Kuna jambo moja ambalo mashabiki wa Twanga Pepeta inabidi walielewe mapema sana kuhusu ujio wa Chocky ndani ya bendi yao – wategemee kazi nzuri kutoka kwake, lakini wasitegemee msisimko wa ajabu. Soko la dansi limegeuka na limemezwa kwa makusudi na bongo fleva.
    Kwa bahati mbaya sana, asilimia 70 ya vituo vya radio vinafanya biashara ya muziki, matamasha makubwa ya muziki ni sehemu ya vitega uchumi vyao hali kadhalika watangazaji wengi nao wanafanya biashara ya muziki aidha kwa kuwa mameneja wa wasanii au kwa kuwa mapromota.
    Katika hali hiyo, ni rahisi zaidi kwa vituo hivyo vya radio ‘kuwamiliki’ na kuwadhibiti wasanii wa kizazi kipya kuliko bendi za dansi ambazo tayari ziko chini ya himaya ya watu wengine huku pia zikiwa zinaundwa na idadi kubwa ya wanamuziki na hapo ndipo tishio la anguko la muziki wa dansi lilipokuja.
    Kwa hali hiyo basi Chocky wa leo hawezi kuwa sawa na Chocky wa “Jirani”, “Chuki Binafisi”, “Busu la Kufunga Mwaka” na “Password” ambazo zilipata muda wa kutosha kwenye vituo vya radio.
    Hilo ni moja, lingine ni ule ukweli usiopingika kuwa msisimko wa Chocky katika enzi hizo ulichagizwa na upinzani wake na Banza Stone – mmoja akiwa Twanga mwingine TOT, baadae mwingine Extra Bongo mwingine Twanga, mara huyu yuko Twanga Pepeta na yule yuko Twanga Chipolopolo.
    Huyu akitoa ‘nondo’ hili yule kajibu kwa ‘nondo’ ile, huyu akipiga dongo hili basi yule atajibu kwa dongo lingine kali. Ilikuwa kama vile wamezaliwa maalum kwaajili ya kuwapa raha Watanzania.
    Ushindani wao ulikufa kifo cha kawaida mwaka 2007 kama sikosei baada ya Twanga Chipopolo iliyokuwa chini ya Banza kuvunjwa halafu Chocky nae akaikimbia Twanga Pepeta na kujiunga na TOT muda mfupi baadae hali iliyoruhusu bendi za FM Academia na Akudo Impact kutawala soko la muziki wa dansi.
    Iliwachukua muda mrefu kidogo Twanga Pepeta kupata ‘fomula’ mpya ya kuwatumia Chaz Baba, Kalala Jr, Khalid Chokoraa na Kupaza kuirejesha bendi kileleni kwa kutoa albam kali ya “Mwana Dar es Salaam”. 
    Kwa sasa Banza ni kama vile ‘amekufa’ kimuziki, Chocky anabaki peke yake bila mtani wake wa jadi, ni kama alivyo Ray hivi sasa bila Kanumba, Ray amebakia kuwa mwigizaji wa kawaida sasa, sio Ray yule ambaye alikuwa hashikiki wakati wa ushindani wake na marehemu Kanumba na ndio maana nasema Chocky bila Banza ni sawa na Ray bila Kanumba.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: ALLY CHOCKY BILA BANZA STONE SAWA NA RAY BILA KANUMBA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top