• HABARI MPYA

  Jumamosi, Aprili 25, 2015

  TAMBWE AKUBALI YAISHE KWA ‘DOGO’ SIMON, ASALIMISHA ‘KIATU CHA DHAHABU’ MAPEMAA

  Na Prince Akbar, DAR ES SALAAM
  MSHAMBULIAJI Amissi Tambwe amekubali yaishe kwa mchezaji mwenzake wa Yanga SC, Simon Msuva kwenye mbio za ufungaji bora wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara.
  Na mfungaji huyo bora wa Ligi Kuu msimu uliopita akiwa na mahasimu, Simba SC amesema hawezi tena kumkamata Msuva.
  Mrundi huyo amesema ni vigumu kwa sasa kumaliza na mabao 19 yaliyompa ufungaji bora msimu uliopita na ‘kiroho safi’ kabisa anamuachia taji Msuva.
  Amissi Tambwe amesema hawezi tena kumkamata Simon Msuva katika mbio za ufungaji bora Ligi Kuu

  Tambwe aliyefunga mabao 11 msimu huu hadi sasa, yakipungua manane kati ya 19 ya msimu uliopita, amesema msimu huu umekuwa mgumu kwake, kutokana na ligi kuwa ngumu kiasi cha kumfanya ashindwe kufikia rekodi yake ya msimu uliopita.
  Mrundi huyo amesema Msuva ambaye anaongoza kwa ufungaji sasa akiwa na mabao 16 baada ya jana kufunga mawili katika ushindi wa 5-0 dhidi ya Ruvu Shooting, ndiye anaweza kufikia rekodi yake endapo ataendelea kufunga.
  "Ligi imekuwa ngumu sana, sidhani kama nitaweza kufikia mabao ya msimu uliopita, lakini nafikiri nafasi hiyo anayo Msuva kama ataendelea kufunga kama sasa,"amesema Tambwe.
  Tambwe amesema Msuva yuko kwenye nafasi nzuri ya kuwa mfungaji bora LIgi Kuu msimu huu

  "Msuva sasa yuko katika nafasi nzuri, anafunga lakini pia kutokana na kuongoza kwake, anaweza kufikia idadi hiyo, bado tuna mechi tatu na amebakiza mabao matatu tu kuifikia,”amesema.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: TAMBWE AKUBALI YAISHE KWA ‘DOGO’ SIMON, ASALIMISHA ‘KIATU CHA DHAHABU’ MAPEMAA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top