• HABARI MPYA

  Tuesday, April 28, 2015

  HANS POPPE: HALI YA KIUCHUMI SI NZURI SIMBA SC, WATU HAWAJI MPIRANI, PATO LIMESHUKA KWA ZAIDI YA ASILIMIA 50

  Na Princess Asia, DAR ES SALAAM
  MWENYEKITI wa Kamati ya Usajili ya Simba SC, Zacharia Hans Poppe amesema kwamba hali ya kiuchumi si nzuri katika klabu hiyo, kutokana na mapato katika mechi zao kushuka kwa zaidi ya asilimia 50.
  Kwa sababu hiyo, Poppe amesema wamejikuta wanaingia kwenye migogoro ya kulipa madeni mbalimbali, lakini hawajadhamiria kumdhulumu yeyote.
  “Hakuna ambaye amekataa kumlipa Tambwe (Amissi). Hayo ni makubaliao yetu sisi na yeye baada ya kumuacha, kwamba tutamlipa kiasi gani. Lakini tatizo hatuna fedha.
  “Mechi zetu za Ligi Kuu kwa sababu ya kuonyeshwa kwenye Televisheni watu wanakuwa hawaji kwa wingi uwanjani. Mgawo wa mapato ya mechi zetu kwa kweli ni aibu. Huwezi kufidia gharama za siku moja tu za kambi,”amesema.
  Poppe ameshauri Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) lijadiliane na Azam TV waliouziwa haki ya kurusha matangazo ya Televisheni ya Ligi Kuu, ili waziongezee fedha klabu kubwa.
  Zacharia Hans Poppe amesema pato la Simba SC limeshuka kwa asilimia 50

  “Ni kweli sisi (Simba na Yanga) tumeathirika kwa sababu ndiyo tuna mashabiki wengi. Huko nyuma kabla ya Azam TV kuanza kuonyesha ligi, tulikuwa tunapata fedha nyingi hata kwenye mechi ndogo tu. Lakini sasa hata ukicheza na timu kama Mtibwa Sugar, Kagera Sugar au Azam mambo magumu,”amesema Poppe.    
  Amesema si sahihi kuwapa Simba na Yanga wenye mashabiki wengi kote nchini mgawo sawa na klabu nyingine na akaishauri TFF, kukutana na Azam TV na kujadili namna ya kuzisaidia klabu hizo kongwe.
  “Sisi tumeathirika mno kwa kweli. Watu hawaji mpira wanakaa tu kwenye maeneo yao wanaangalia Azam TV,”amesema.
  Simba SC inakabiliwa na madeni mbaimbali kutoka kwa waajiriwa wake iliyowaondoa kazini kama kocha Mcroatia Zdravko Logarusic ambaye anadai Sh. Milioni 112.
  Logarusic alifukuzwa Simba SC Agosti mwaka jana kiasi cha mwezi mmoja baada ya kusaini Mkataba mpya na klabu hiyo, baada ya ule wa awali wa majaribio wa miezi sita ulioanza Desemba 2013 kumalizika.
  Na mwalimu huyo ambaye kwa sasa anafundisha AFC Leopard ya Kenya, anataka alipwe dola 6,000 ambazo ni mshahara wake wa mwezi mmoja, Agosti na dola 50,000 kwa kuvunja mkataba.
  Kesi hiyo ilitarajiwa kusikilizwa juzi mbele ya Kamati Sheria na Hadhi za Wachezaji chini ya Mwenyekiti Richard Sinamtwa, lakini ikashindikana kutokana na mapungufu kadhaa na sasa itapangiwa siku nyingine. 
  Upande wa Simba SC uliowakilishwa na Katibu wake, Stephen Ally uliomba uthibitisho kwa mwakilishi wa Logarusic katika kesi hiyo kama kweli ameagizwa na kocha huyo, lakini ukakosekana.
  Wakili wa Loga akaambiwa aende kupata uthibitisho wa kupewa jukumu la kumuwakilisha Mcroatia huyo na baada ya hapo, kesi itaanza kusikilizwa.
  Aidha, kiungo wa Simba SC, Haroun Chanongo anayecheza kwa mkopo Stand United ya Shinyanga naye ameishitaki klabu hiyo. 
  Chanongo anadai wakati anapelekwa kwa mkopo Stand United Novemba mwaka jana, makubaliano yalikuwa ni kila klabu ilipe nusu katika mshahara wake.
  Hata hivyo, Chanongo amesema kwamba tangu anodoke Simba SC hajawahi kupewa nusu mshahara wake, wakati wa Stand anaendelea ‘kukunja’ kama kawaida bila mushkeli. 
  Madai ya Tambwe ni jumla ni dola za Kimarekani 7,000 (Sh. Milioni 14 za Tanzania), kati ya hizo 1,000 zikiwa ni mshahara wa mwezi mmoja na nyingine za kuvunjia Mkataba.
  Simba SC wamepewa hadi Aprili 30 kuwa wamemlipa Tambwe dola 5,000 na nyingine wamalizie Mei 10, mwaka huu- na wakishindwa kufanya hivyo watakatwa fedha zote mara moja katika mapato ya mechi zao.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: HANS POPPE: HALI YA KIUCHUMI SI NZURI SIMBA SC, WATU HAWAJI MPIRANI, PATO LIMESHUKA KWA ZAIDI YA ASILIMIA 50 Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top