• HABARI MPYA

  Tuesday, April 28, 2015

  BIN SLUM ‘AZIMWAGA’ NDANDA, STAND UNITED…MBEYA CITY WAPEWA NAFASI YA MWISHO

  Na Prince Akbar, DAR ES SALAAM 
  MKURUGENZI wa kampuni ya Bin Slum Tyres Limited, Nassor Bin Slum amesema kwamba hataongeza Mkataba na klabu za Ndanda FC ya Mtwara na Stand United ya Shinyanga.
  Bin Slum aliingia Mkataba na Ndanda na Stand zote zilizopanda Ligi Kuu msimu huu wa mwaka mmoja, kwa dau la Sh. Milioni 50 kwa kila timu.
  Lakini wakati msimu unaelekea ukingoni na bingwa amekwishaptikana, Yanga SC, Bin Slum amesema hataendelea na timu hizo.
  Akizungumza na BIN ZUBEIRY jana Dar es Salaam Nassor alisema kwamba aliamua kuzidhamini timu hizo ili kuwahamasisha wafanyabiashara wengine pia wajitokeze kudhamini timu mbalimbali.
  Wamepigwa chini; Nassor Bin Slum (kulia) wakati anasaini Mkataba na Ndanda FC mwaka jana

  “Kwa hiyo baada ya kutoa changamoto hiyo nzuri, nadhani ni fursa sasa kwa wafanyabiashara wengine hata wa pale pale Mtwara na Shinyanga pia, kujitokeza kudhamini timu zao,”amesema.
  Bin Slum ambaye pia ni mdhamini wa Mbeya City kwa dau la Sh. Milioni 250 amesema kuhusu timu hiyo ya Halmshauri ya Jiji la Mbeya wao aliingia nao Mkataba wa miaka miwili.
  “Mbeya City niliingia nao Mkataba wa miaka miwili. Sasa tusubiri tuone mwaka wa pili wa Mkataba wetu, ndiyo tutasema kama tutaendelea au la, ila kwa sasa mapema sana,”alisema Bin Slum.
  Mfanyabiashara huyo mzalendo na kijana, aliweka rekodi nchini mwaka jana baada ya kuingia Mkataba wa kuzidhamini klabu tatu kwa mpigo za Ligi Kuu, Stand waliokuwa wanamtangazia tairi za Vee Rubber, Ndanda tairi za Double Star na Mbeya City betri za RB.
  Umaarufu wa Bin Slum ulianzia alipokuwa mfadhili Mkuu wa Coastal Union kwa miaka minne hadi mwaka jana, kabla ya kutofautiana na uongozi na kuamua kujiweka kando.
  Lakini bado Bin Slum amekuwa akisaidia timu nyingine nchini mfano Villa Squad na Coastal Union- pamoja kuwasaidia wanamichezo mbalimbali wanaobahatika kumfikia.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: BIN SLUM ‘AZIMWAGA’ NDANDA, STAND UNITED…MBEYA CITY WAPEWA NAFASI YA MWISHO Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top