• HABARI MPYA

  Thursday, April 23, 2015

  RWANDA WAIKATAA CHALLENGE, WAZIRI ASEMA WANA CHAN 2016

  Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
  MICHUANO ya Kombe la Mataifa ya Afrika Mashariki na Kati CECAFA Challenge kwa mwaka wa pili mfululizo iko shakani kufanyika, kufuatia Serikali ya Rwanda kuukana uenyeji.
  Taarifa ya Wizira ya Michezo na Utamaduni wa Rwanda, imesema kwamba Serikali haiko tayari kupokea uenyeji wa Challenge, kwa kuwa tayari ina mzigo wa kuandaa CHAN mwakani.
  Taarifa hiyo imesema Shirikisho la Soka la Rwanda limekubaliana na CECAFA juu ya kuandaa Challenge bila kuwasiliana na Wizara yake, jambo ambalo ni kosa.
  Wazi FERWAFA bila msaada wa Serikali haiwezi kumudu gharama za kuandaa Challenge- maana yake michuano hiyo kwa mwaka mwingine tena huu, iko shakani kufanyika.

  Hatuitaki Challenge, tuna CHAN;  Waziri wa Michezom na Utamaduni wa Rwanda, Julienne Uwacu. Wizara yake imesema haiko tayari kwa uenyeji wa Kombe la Challenge 2015

  FERWAFA ilitaka sana uenyeji wa Challenge ili kukiandaa kikosi chake cha CHAN mwakani na pia kujiandaa kwa ujumla na mikiki na Michauno ya Ubingwa wa Mataifa ya Afrika, inayohusisha wachezaji wanaocheza ligi za nchini mwao pekee.    
  Mwaka jana, CECAFA ilishindwa kufanya Challenge kufuatia Ethiopia waliopewa uenyeji kujitoa dakika za mwisho na Baraza hilo la Vyama vya Soka Afrika Mashariki na Kati likakosa nchi nyingine ya kuyapokea mashindano hayo. 
  Wakati huo huo, michuano ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, Kagame nayo pia iko kwenye hatihati kufanyika mwaka huu kutokana na Tanzania waliopewa uenyeji kutohibitisha hadi sasa.
  CECAFA ilitaja wenyeji wa michuano yake wiki iliyopita, Rwanda Challenge na Tanzania Kombe la Kagame, lakini Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) likasema limepokea maombi ya kuandaa mashindano hayo na watayajadili.
  CECAFA kwa sasa inaonekana kuelemewa na mzigo wa kuandaa mashindano yake, kutokana na nchi wanachama wake kukwepa uenyeji kwa kuhofia gharama- tatizo kubwa likiwa ni kukosekana kwa wadhamini wa kubeba gharama za mashindano.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: RWANDA WAIKATAA CHALLENGE, WAZIRI ASEMA WANA CHAN 2016 Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top