• HABARI MPYA

  Jumatatu, Aprili 27, 2015

  TENGA: PELEKENI SOKA MASHULENI, HALI MBAYA

  Na Prince Akbar, DAR ES SALAAM
  MWENYEKITI wa Baraza la Vyama vya Soka Afrika Mashariki na Kati (CECAFA), Leodegar Tenga ameshauri soka ifundishwe zaidi mashuleni, kwa sababu hali ni mbaya katika soka ya Tanzania hivi sasa na lazima jitihada zinahitajika ili kuweka mambo sawa.
  Akizungumza wakati wa ufunguzi wa kozi ya Wakufunzi wa Makocha wa madaraja ya juu asubuhi ya leo Uwanja wa Karume, Dar es Salaam, Tenga amesema kwamba Wakufunzi wa Makocha wanapaswa kufanya kazi ya kuzalisha makocha wengi.
  “Kwa sasa hapa Tanzania hatuna timu za watoto 500, timu kwa maana ya timu ina makocha, vifaa na wanaandaliwa kwa kufundishwa angalau mara moja kwa wiki. Hatuna,”.
  “Sisi hapa tuna desturi ya kukutanisha watoto siku chache kabla ya mashindano, wanafanya mazoezi tu, basi. Na hilo ni tatizo la nchi nyingi Afrika, kwa kweli bado tupo nyuma sana na tuna kazi kubwa ya kufanya,”amesema.   
  Leodegar Tenga (kushoto) akizungumza leo pembeni ya Rais wa TFF, Jamal Malinzi
  Tenga ameipongeza TFF, (Shirikisho la Soka Tanzania) kwa kufanya kozi ya Wakufunzi wa Makocha na akasema wanafuata mwongozo wa Shirikisho la Soka Afrika (CAF).
  “Hatuna namna nyingine ya kufanya. Lazima tukimbie wakati wenzetu wanatembea, wenzetu wametuacha mbali sana. Kungekuwa na Kombe la Dunia la nchi dhaifu kisoka, tusingekuwa na haja ya kuendesha mafunzo, lakini kwa sababu hakuna, lazima tufanye hivi,”amesema Tenga.   
  Tenga amempongeza Rais wa TFF, Jamal Malinzi kwa kuwa muumini wa soka la vijana na kasema lazima mpira uchezwe mno mashuleni.
  “Tuzalishe wakufunzi bora, wakazalishe makocha ambao watakwenda kufundisha watoto. Hapo tutakuwa na matumaini,”amesema Tenga.  
  Tenga, beki wa zamani wa Yanga SC na Taifa, Stars aliyewahi pia kuwa Nahodha wa Taifa Stars, ni miongoni mwa washiriki wa kozi hiyo, wengine wakiwa ni kocha wa zamani wa Taifa Stars, Profesa Mshindo Msolla, Michael Bundala, George Komba na Oscar Don Korosso.
  Wamo pia Wilfred Kidao, Rogasian Kaijage, Mkisi Samson, Ally Mtumwa, Madaraka Bendera, Juma Nsanya,  Hamim Mawazo, Wanne Mkisi, Meja Abdul Mingange, Dk. Jonas Tiboroha, Nasra Mohamed, John Simkoko, Juma Mgunda, Triphonia Temba, Ambonisye  Florence, na Eugen Mwasamaki.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: TENGA: PELEKENI SOKA MASHULENI, HALI MBAYA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top