• HABARI MPYA

  Jumatano, Aprili 29, 2015

  MALINZI AFANYE YOTE, LAKINI AJUE NA HILI NI MUHIMU MNO KWA USTAWI WA SOKA YETU

  BINGWA wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, msimu wa 2014/2015 amekwishapatikana, Yanga SC. 
  Yanga imetwaa taji lake la 24 la Ligi Kuu kufuatia ushindi wa mabao 4-0 dhidi ya Polisi Moro Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam Jumatatu.
  Matokeo hayo yanaifanyA Yanga SC ifikishe pointi 55 ambazo haziwezi kufikiwa na timu nyingine yoyote katika ligi hiyo.
  Hilo linakuwa taji la 24 la Ligi Kuu kwa Yanga SC, baada ya awali kulitwaa katika miaka ya 1968, 1969, 1970, 1971, 1974, 1981, 1983, 1985, 1987, 1989, 1991, 1992, 1993, 1996, 1997, 1998, 2002, 2005, 2006, 2008, 2009, 2011 na 2013.
  Kwa kawaida, Ligi Kuu huanza mwishoni mwa Agosti au Septemba mwanzoni na kufika Novemba, au Desemba mzunguko wa kwanza unakamilika. Maana yake mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu unachezwa kwa miezi miwili au mitatu- tumemaliza kazi.

  Baada ya hapo wachezaji wanakwenda kupumzika hadi watakaporejea kwenye mzunguko wa pili wa Ligi Kuu, mwishoni mwa Januari au mwanzoni mwa Februari.
  Na kutoka hapo watacheza mzunguko huo wa pili wa Ligi Kuu ya timu 14 hadi mwishoni mwa Aprili au mapema Mei, ligi inakuwa imemalizika na bingwa amekwishapatikana, timu za kushuka Daraja zimekwishajulikana.
  Siri kubwa ya kufanikiwa kumaliza ligi haraka ni kuikimbiza, kuichezesha haraka kila wiki, kila timu inacheza wastani wa mechi mbili au tatu.
  Tumeona Yanga SC ilivyokimbizwa katika mechi tatu za mwisho kuelekea ubingwa, ilicheza  Jumanne na Stand United ikashinda 3-2, ikacheza Ijumaa na Ruvu Shooting ikashinda 5-0 na ikacheza Jumatatu na Polisi ikashinda 4-1.
  Pamoja na miundombinu yetu mibovu, lakini bado tumeshuhudia timu ikisafiri kutoka kituo kimoja hadi kingine mara tatu ndani ya wiki moja.
  Tutakapokamilisha kabisa msimu huu wa Ligi Kuu, wachezaji wasiozidi 20 watakwenda timu ya taifa, Taifa Stars kwa ajili ya michuano ya COSAFA mwezi ujao nchini Afrika Kusini.
  Wachezaji wengine wa klabu za ligi hiyo hawatakuwa na mashindano mengine yoyote ya kushiriki hadi watakaporudi kwenye ligi Agosti au Septemba.
  Unaweza ukajiuliza iko wapi faida ya kuikimbiza Ligi Kuu kwa kasi hiyo ikiwa hakuna mashindano mengine mbele? Kitaalamu, mchezaji anatakiwa kucheza sana ili kuwa fiti, lakini kwa mchezaji wa Tanzania anayecheza Ligi Kuu kwa miezi minne hadi sita ya msimu, unatarajia nini?
  Hiyo ni nchi ambayo haina wachezaji wanaochwza Ligi kubwa Ulaya na bado watu wake wana ndoto za kuishuhudia timu yao ya taifa katika michuano mikubwa kama AFCON na Kombe la Dunia.
  Kijasho chembamba kinatutoka kupangwa na Nigeria, Chad na Misri kufuzu AFCON na wakati huo huo tumepangiwa kuanza na Uganda kufuzu CHAN.
  Ndiyo maana kila siku klabu zetu zinawamezea mate wachezaji wa nchi jirani kama Kenya na Uganda, kwa sababu wanacheza Ligi ndefu na bado wana mashindano mengine kama Kombe la FA na kadhalika.
  Sisi ukisikia mashindano mengine ni ya ujanja ujanja tu ya wiki mbili mbili kama Kombe la Mapinduzi kule Zanzibar, sasa saa ngapi unategemea kumjenga mchezaji katika kiwango cha ushindani?
  Hapo hapo unamsikia mtu mwingine anahoji, hivi kwa nini wachezaji wa Taifa Stars watoke Azam, Simba na Yanga pekee, hakuna timu nyingine?
  Anasahau kwamba Azam, Simba na Yanga ndizo ambazo kwanza zinasajili wachezaji waliong’ara kutoka timu nyingine- na pili ndizo ambazo zinacheza mechi nyingi kidogo kuliko timu nyingine.
  Kutoka timu hizo tatu ndipo hupatikana wawakilishi wa Tanzania kwenye Kombe la Kagame, Ligi ya Mabingwa Afrika hata Kombe la Shirikisho- sasa kwa vyovyote lazima mchezaji wa timu ya taifa atokane na timu hizo.
  Naziona jitihada za rais mpya wa TFF, Jamal Emil Malinzi katika kuhakikisha analeta mabadiliko kwenye soka ya Tanzania na kwa hakika anaonyesha matumaini.
  Malinzi alipoingia madarakani alitamka dhamira yake ya kurejesha mashindano ya Kombe la FA ambayo yatawapa fursa zaidi wachezaji wa klabu zetu.
  Nchi nyingi Afrika zina mashindano mengine baada ya Ligi Kuu, ambayo uzito wake ni kutoa mwakilishi wa nchi katika michuano ya pili kwa ukubwa barani.
  Uganda na Kenya wote hawapati wawakilishi wa Kombe la Shirikisho kutokana na Ligi Kuu kama ilivyo sisi hapa, bali hutokana na mashindano mengine yanayoandaliwa na FA zao.
  Miaka ya nyuma Tanzania ilikuwa na mashindano ya FA na yalitoa wawakilishi wa Kombe la Shirikisho na Kombe la Washindi enzi hizo, lakini sasa yamekufa, hayapo.
  Kwa sasa kila klabu ya Ligi Kuu ina timu ya vijana U20, wazi kama hayo mashindano yatakuwepoo makocha watatumia wachezaji wa timu hizo japo katika hatua za awali.
  Pamoja na hayo, kuna wachezaji bora wanaosajiliwa na klabu za Ligi Kuu, lakini wakakosa nafasi kwenye vikosi vya kwanza kutokana na kuzidiwa uwezo na wenzao- hawa wanaweza kupata nafasi ya kucheza kama kutakuwa na Kombe la FA.
  Katika mipango yake ya kuipeleka juu soka ya Tanzania, Malinzi asisahau kwamba na hili la Kombe la FA ni muhimu mno kwa ustawi wa mchezo huo nchini. 
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: MALINZI AFANYE YOTE, LAKINI AJUE NA HILI NI MUHIMU MNO KWA USTAWI WA SOKA YETU Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top