• HABARI MPYA

  Jumatano, Aprili 29, 2015

  MALINZI AELEZEA DIRA YA OLIMPIKI 2020

  Na Prince Akbar, DAR ES SALAAM
  RAIS wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Jamal Malinzi amesema dira yake ni kuiona timu ya taifa ya vijana chini ya umri wa miaka 23 inacheza Fainali za Olimpiki za mwaka 2020 mjini Tokyo, Japan,
  Katika mahojiano maalum na BIN ZUBEIRY juzi, Malinzi amesema programu ya kutengeneza timu ya kucheza Olimpiki ya Tokyo 2020 imekwishaanza.
  Malinzi amesema kikosi cha taifa cha wachezaji chini umri wa miaka 15 kilichoundwa kutokana na nyota wa mashindano ya Copa Coca Cola tayari kipo kambini chini ya kocha Mohammed ‘Adolph’ Rishard.

  Malinzi amesema kikosi hicho kinaandaliwa ili kicheze Fainali za U17 Afrika mwaka 2017 nchini Madagascar.
  Amesema baada ya hapo wachezaji hao wataendelea kukuwa kisoka na kupanda katika madaraja mengine ya mashindano ya vijana, U20 na baadaye U23.
  “Lengo kuu, mwaka 2020 tucheze Olimpiki ya Tokyo. Na kama tutakwenda Tokyo na wachezaji hawa tunaowaandaa sasa, naamini wanaweza kutupeleka AFCON na Kombe la Dunia baada ya hapo,”amesema Malinzi.
  Amesema kikosi cha Adolph Desemba mwaka huu kitazuru Malawi, Zambia, Zimbabwe, Botswana na Afrika Kusini kucheza mechi za kirafiki na U17 za huko.
  Amesema Aprili mwakani watoto hao watakwenda Burundi, Rwanda, Uganda na Kenya kucheza na U17 za huko pia na baada ya hapo wataingia kambini kujiandaa na mechi za mtoano kuelekea Madagascar 2017.
  Aidha, Malinzi amesema Tanzania imeomba uenyeji wa michuano ya U17 mwaka 2019, hiyo ikiwa programu ya pili ya vijana, baada ya hii ya sasa.
  “Mchakato wa kuwapata U17 wa kucheza Fainali za 2019 kama tutapewa umekwishaanza, tutaanza na mashindano ya U13 pale Mwanza,”amesema.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: MALINZI AELEZEA DIRA YA OLIMPIKI 2020 Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top