• HABARI MPYA

  Jumapili, Aprili 26, 2015

  NCHI ZIGOMEE COSAFA KULAANI MAUWAJI DHIDI YA RAIA WA KIGENI AFRIKA KUSINI

  WAKATI Shirikisho la Soka Afrika Kusini (SAFA) linaendelea na maandalizi ya michuano ya Mataifa ya Kusini mwa Afrika, COSAFA amani imepotea nchini humo.
  Hiyo inafuatia kuibuka kwa mashambulizi dhidi ya raia wa kigeni nchini Afrika Kusini, yaliyoibua ghasia zilizosababisha wahamiaji zaidi ya 5,000 kukosa makazi.
  Vurugu na mauaji dhidi ya wageni nchini Afrika Kusini zimesambaa kutoka mji wa bandari wa mashariki wa Durban hadi mji mkuu wa kiuchumi wa taifa hilo, Johannesburg mwezi huu.
  Shirika la Wakimbizi la Umoja wa Mataifa (UNHCR) limesema zaidi ya raia wa kigeni 5,000 wakiwemo wakimbizi wameachwa bila makazi nchini humo kutokana na vurugu hizo.

  Shirika hilo limesisitiza kwenye taarifa yake kwamba waathirika wa ghasia hizo ni pamoja na wakimbizi, ambao wamelazimika kuzikimbia nchi zao kutokana na vita na kuhofia kukamatwa na kushitakiwa na kwa hivyo wapo Afrika Kusini kwa sababu wanahitaji kulindwa.
  Katika muda wa wiki mbili zilizopita maduka pamoja na majumba yanayomilikiwa na wahamiaji kutoka Somalia, Ethiopia, Malawi, Msumbiji, Zambia, Zimbabawe na wengine mjini Durban wakiwemo Watanzania, wamelengwa katika mashambulio hayo, hali iliyozilazimu familia nyingi kukimbilia katika makambi yanayolindwa na walinzi wenye silaha.
  Maduka ya wageni katika mji wa Jeppes, Johannesberg pia yameshambuliwa. Ikumbukwe kwamba wenyeji na wahamiaji nchini humo mara kwa mara hushindania ajira hali ambayo mara zote inawafanya wageni kulengwa katika vurugu za aina hii pamoja na uchokozi mwingine.
  Mwaka 2008 watu 62 waliuwawa katika vurugu na ghasia zinazotokana na chuki dhidi ya wageni katika mitaa ya mji wa Johannesberg.
  Ghasia hizi mpya zinazoshuhudiwa zilizuka baada ya mfalme wa Zulu Goodwill Zwelithini kutoa matamshi kwenye vyombo vya habari vya ndani kwamba wageni wanapaswa kuondoka Afrika Kusini.
  Hata hivyo, tangu wakati huo amenukuliwa akisema kwamba kauli yake ilitafsiriwa vibaya.
  Ghasia hizo zimeendelea kupingwa duniani. Jumuiya ya kiuchumi ya nchi za Magharibi mwa Afrika ECOWAS imelaani mauaji na vurugu hizo ikisema ni kitendo kilichopitwa na wakati, cha kihalifu na mauaji ya chuki dhidi ya wageni wasiokuwa na hatia nchini humo.
  Jumuiya hiyo Imeitaka serikali ya Afrika Kusini kuchukua hatua za haraka kukomesha kuongezeka kwa wimbi hilo la mashambulizi nchi nzima.
  Rais wa Ghana John Dramani Mahama akitoa taarifa kwa niaba ya ECOWAS kama Mwenyekiti wake, amesema Afrika Kusini inabidi itambue wanaouwawa kwa kuonekana ni watu kutoka nje ni watu ambao nchi zao zilijitolea kuwasaidia Waafrika Kusini kupambana, kuzuia na kuushinda ubaguzi wa rangi. Mapema wiki hii Malawi ilitangaza itawaondoa raia wake wanaishi Afrika Kusini. Alhamisi mamia ya watu waliandamana hadi ofisi za ubalozi wa Afrika Kusini mjini Harare Zimbabwe kupinga mashambulizi hayo. 
  Afrika Kusini kupitia Waziri wake wa Mambo ya nje Maite Nkoana-Mashabane aliyekuwa na Mkutano na Wanadiplomasia wa Kiafrika mjini Pretoria, imeomba uungaji mkono wa kidiplomasia wa nchi za Kiafrika kukabiliana na hali hii.
  Wakati hali ikiwa mbaya kiasi hicho Afrika Kusini, SAFA bado wana matumaini ya kuwa wenyeji wa COSAFA ya mwaka huu mwezi ujao, ambayo itashirikisha na nchi za Ghana na Tanzania ambao si wanachama wa COSAFA, walioshirikishwa kuongeza ladha ya mashindano.
  Lakini timu zote zitakazokwenda Afrika Kusini ni ambazo raia wake wananyanyaswa na kuuawa nchini humo.
  Hakika litakuwa jambo la ajabu, iwapo Msumbiji, Zimbabwe, Zambia, Malawi, Tanzania na hata Ghana zikipeleka vikosi vyake Afrika Kusini kwa ajili ya COSAFA.
  Waafrika Kusini sasa wanapaswa kupewa somo, kufikishiwa ujumbe kwamba walichokifanya si sahihi na hawaijui kabisa historia.
  Wamesahau kwamba Afrika yote iliungana kuhakikisha Afrika Kusini inajitoa kwenye mbavu za Makaburu na kuwa nchi huru- leo wanawanyanyasa wale wale waliowasaidia.
  Mkoa wa Morogoro, Tanzania ndiyo makao makuu ya kwanza ya chama cha ANC uhamishoni, kabla ya ANC kuhamia Lusaka, Zambia.
  Mwaka 1976, baada ya kutokea mauaji makubwa ya wanafunzi katika mji wa Soweto, yaliyotekelezwa na polisi wa makaburu, na hivyo kusababisha vijana wengi wa ANC kuikimbia Afrika Kusini na kwenda kuwa wakimbizi nje, chama hicho kiliona haja ya kuwa na shule yake nchini Tanzania ambayo ingetumiwa na vijana hao wa ANC waliokuwa wamekimbia kukwepa vipigo vya Polisi.
  Kutokana na hali hiyo, mwaka huo, ujumbe wa ANC uliwasilisha ombi kwa baba wa taifa, Mwalimu Julius Nyerere la kupatiwa ardhi ya kutosha ya kuweza kujenga shule zake, kuanzia chekechea, msingi na sekondari. 
  Mwalimu alikubali ombi hilo la ANC na kuwakabidhi wajumbe hao kwa Mkuu wa Mkoa wa Morogoro wa wakati huo, Anna Abdallah ili awatafutie ardhi ndani ya mkoa wake.
  Anna Abdallah, aliwachukua viongozi hao wa ANC, akiwamo Tambo hadi katika shamba la mkonge la Mazimbu na kuwakabidhi eneo hilo kwa ajili ya kuanzisha Kituo cha Elimu cha ANC (ANC Education Facilities). 
  Mwaka 1978 ilizinduliwa rasmi shule ya kwanza ya msingi ya ANC Mazimbu, mwalimu wake mkuu akiwa Wintshi Njobe.
  Mwaka 1979, ANC ilipata pigo kubwa baada ya mwanaharakati wake kijana, mwanafunzi bado wa shule, ambaye alikuwa mwiba kwa serikali ya kibaguzi ya makaburu, Solomon Mahlangu, kunyongwa hadi kufa baada ya Mahakama ya nchi hiyo kumtia hatiani na kutoa hukumu ya kunyongwa mwaka 1977, kwa madai ya kuendesha vitendo vya kigaidi.
  Inasimuliwa kwamba wakati wa kutekeleza hukumu hiyo ya kunyongwa, Aprili 6, mwaka 1979, akiwa katika Gereza Kuu la Pretoria, makaburu walimwita mama yake na ndugu yake ili kushuhudia tukio hilo la kinyama.
  Wakati Solomon akipandishwa kwenye kitanzi, kijana aliyekuwa amehitimu mafunzo ya Umkhonto wa Sizwe katika kambi za jeshi za ANC nchini Angola na Msumbiji kutokana na kukatishiwa masomo yake na Makaburu akiwa darasa la nane mwaka 1976, mama yake alianza kububujikwa machozi, lakini Solomon akamwambia mama yake kwamba hakuwa na sababu yoyote ya kulia, na badala yake akamwambia mama yake maneno yafuatayo:
  “Tell my people that I love them and that they must continue the struggle, my blood will nourish the tree that will bear the fruits of freedom. Aluta Continue.” (Mama ninakufa, waambie watu wangu (Wana-ANC) kwamba nawapenda na waendeleze mapambano haya, damu yangu hii itakayomwagika ndiyo itakuwa kirutubisho cha mti ambao hatimaye utatoa matunda ya uhuru. Mapambano yanaendelea).
  Baada ya tukio hilo la kunyongwa kwa mwanafunzi Solomon aliyekuwa na miaka 23, kituo cha elimu cha ANC Mazimbu, Morogoro, kilibadilisha jina la kituo hicho kama hatua ya kumuenzi mwanaharakati huyo, na kukiita Solomon Mahlangu Freedom College (Somafco) hadi mwaka 1992 kilipofungwa baada ya utawala wa makaburu kusalimu amri dhidi ya harakati za ANC, kwa kumwachia huru Nelson Mandela kutoka kifungo cha maisha, kuruhusu shughuli za kisiasa, kisheria na mfumo wa demokrasia ya vyama vingi, na hivyo kutimia kwa ndoto ya Solomon Mahlangu.
  Solomon Mahlangu Campus, SUA Kwa sasa eneo hilo la Somafco Mazimbu, linamilikiwa na Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine (SUA), baada ya Serikali kulikabidhi rasmi kwa chuo hicho mwaka 1998.
  Historia inaeleza namna ambavyo nchi mbalimbali ambazo leo raia wake wanafukuzwa kwa mitutu na mapanga Afrika Kusini zilivyosaidia harakati za ukombozi wa nchi hiyo.
  Tunaweza kufanya nini kuwafikishia ujumbe Waafrika Kusini? Kwanza tugomee COSAFA. 
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: NCHI ZIGOMEE COSAFA KULAANI MAUWAJI DHIDI YA RAIA WA KIGENI AFRIKA KUSINI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top