• HABARI MPYA

  Jumatano, Aprili 29, 2015

  TFF YAKWAMA KUTOA NYASI BANDIA ZA MSAADA FIFA BANDARINI

  Na Prince Akbar, DAR ES SALAAM
  SHIRIKISHO la Soka Tanzania (TFF) limekwama kutoa nyasi bandia Bandarini, Dar es Salaam za msaada kutoka Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA) kutokana na kushindwa kulipa ushuru na kodi.
  TFF iliomba nyasi hizo kwa ajili ya kuziweka kwenye viwanja vya Nyamagana, Mwanza na Kaitaba, Bukoba na Rais wa shirikisho hilo, Jamal Malinzi amesema zimekuja tayari, lakini wamekwama kuzitoa.
  “Tumekwama kwa sababu ya kodi. Hatuna fedha. Tunaomba msamaha wa Serikali, itusamehe kama ilivyokuwa kwa nyasi za Uwanja wa Gombani, Karume na Uhuru,”amesema Malinzi.
  Rais wa TFF, Jamal Malinzi kushoto ameomba Serikali iwasadie msamaha wa kodi za vifaa vya michezo 

  Malinzi amesema kwamba wamekuwa wakikutana na vikwazo vingi vya kutoa vifaa vya michezo wanavyopata kwa msaada kutokana na kodi.
  “Tunahitaji vifaa vingi vya michezo tusambaze mashuleni mpira uchezwe. Na tunaomba misaada kwa bahati nzuri tunapata, lakini vikiingia hapa, tunatakiwa tuvilipie kodi na sisi hatuna fedha,”amesema Malinzi.
  Malinzi amemuomba Waziri wa Habari Utamaduni na Michezo, Dk Fenella Mukangara kuisaidia TFF iweze kusamehewa kodi ya vifaa vya michezo kwa manufaa ya mchezo huo nchini.
  “Hivi si vitu ambavyo tunavifanyia biashara. Hivi ni vitu kwa ajili ya maendeleo ya soka nchini. Kwa sasa tuna programu nyingi za vijana, zinahitaji vifaa vingi, vijana waandaliwe waje kuijengea heshima nchi yetu katika soka baadaye. Tunaomba Serikali itusaidie katika hilo,”amesema Malinzi.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: TFF YAKWAMA KUTOA NYASI BANDIA ZA MSAADA FIFA BANDARINI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top