• HABARI MPYA

    Monday, April 27, 2015

    YANGA ‘FULL SHANGWE’ DAR MPAKA MIKOA...POLISI WAPELEKA KOMBE JANGWANI

    Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
    YANGA BINGWA. Naam, taji la 25 la ubingwa wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara limekwenda makutano ya mitaa ya Twiga na Jangwani, yalipo makao makuu ya klabu ya Yanga SC, likitoka Chamazi, Mbade yalipo maskani ya Azam FC.
    Yanga SC imeivua ubingwa Azam FC jioni hii kufuatia ushindi wa mabao 4-1 dhidi ya Polisi Moro Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam- hivyo kufikisha pointi 55 ambazo haziwezi kufikiwa na timu nyingine yoyote katika ligi hiyo.
    Kocha Mkuu wa Yanga SC, Mholanzi Hans van der Pluijm na Msaidizi wake, Charles Boniface Mkwasa walikuwa wenye furaha leo kutokana na kazi nzuri ya vijana wao, soka safi na mabao.
    Hilo linakuwa taji la 24 la Ligi Kuu kwa Yanga SC, baada ya awali kulitwaa katika miaka ya 1968, 1969, 1970, 1971, 1972, 1974, 1981, 1983, 1985, 1987, 1989, 1991, 1992, 1993, 1996, 1997, 1998, 2002, 2005, 2006, 2008, 2009, 2011 na 2013.
    Amisi Tambwe alikabidhiwa mpira wake baada ya kufunga hat trick leo

    Katika mchezo huo uliochezeshwa na refa Zacharia Jacob wa Pwani aliyesaidiwa na Hassan Zani na Abdallah Uhako wote wa Arusha, hadi mapumziko Yanga SC walikuwa mbele kwa bao 1-0.
    Bao zuri lilifungwa na mshambuliaji wa kimataifa wa Burundi, Amissi Tambwe dakika ya 40 akimalizia krosi ya winga Simon Msuva. 
    Dakika nane baada ya kuanza kipindi cha pili, Mrundi huyo aliifungia Yanga SC bao la pili akiuwahi mpira uliotemwa na kipa Abdul Ibadi kufuatia krosi ya Msuva.
    Mfungaji huyo bora wa Ligi Kuu msimu uliopita akiwa na Simba SC, Tambwe akakamilisha hat-trick yake dakika ya 59 akiunganisha vizuri krosi ya Mrisho Ngassa- hilo likiwa bao lake la 14 msimu huu.
    ‘Golden Boy’, Mrisho Khalfan Ngassa akamsetia na Msuva kufunga bao la nne la la 17 kwake msimu huu, akiendelea kuongoza mbio za ufungaji bora.
    Bantu Admin aliifungia Polisi bao la kufutia machozi dakika ya 83 na Tambwe alikabidhiwa mpira baada ya mechi, hiyo ikiwa hat trick ya pili anafunga msimu huu pekee.
    Baada ya mechi shangwe za ubingwa zilianza, mashabiki wa Yanga wakiandama kuanzia Uwanja wa Taifa hadi mitaa mbalimbali, ni nderemo na vifijo tu.
    Mrisho Ngassa wa Yanga SC akipambana na Said Mkangu wa Polisi leo
    Simon Msuva akipasua katikati ya wachezaji wa Polisi leo

    Hali iko hivyo pia kwa mikoa mbalimbali ya Bara na visiwani, mashabiki wa Yanga wakisherehekea ubingwa 24.
    Kikosi cha Yanga SC kilikuwa; Deo Munishi ‘Dida’, Juma Abdul, Oscar Joshua, Mbuyu Twite, Kevin Yondan, Said Juma, Simon Msuva/Hussein Javu dk75, Haruna Niyonzima, Amissi Tambwe/Jerry Tegete dk75, Mrisho Ngassa na Kpah Sherman. 
    Polisi Moro; Abdul Ibad, Hassan Mganga, Ally Teru, Meshack Abel, Laban Kambole, Anafi Suleiman, Bantu Admin, Said Mkangu, Said Bahanuzi/Nicholas Kabipe dk51, Suleiman Kassim ‘Selembe’ na James Ambrose/Mussa Mohamed dk78.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: YANGA ‘FULL SHANGWE’ DAR MPAKA MIKOA...POLISI WAPELEKA KOMBE JANGWANI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top