• HABARI MPYA

    Thursday, December 03, 2020

    WIZARA YAWATAKA WASANII WA BONGO FLEVA KUWASILISHA SERIKALINI MAHITAJI YA KUBORESHA TASNIA YA MUZIKI

    Na Anitha Jonas – WHUSM, DAR ES SALAAM
    KATIBU Mkuu Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na Msemaji Mkuu wa Serikali Dkt. Hassan Abbasi amewataka Wasanii wa Bongo Fleva kuandaa mambo muhimu wanayotaka Serikali iwafanyie ili kuboresha tasnia hiyo.
    Dkt. Abbasi ametoa kauli hiyo Leo Desemba 1, 2020 Jijini Dar es Salaam, katika kikao na Wasanii wa Bongo Fleva nchini, ambapo kikao hicho  kililenga kujadilia namna bora ya kuisaidia tasnia hiyo kunufaika na kazi zake na kuweka mikakati bora ya kukuza kuendeleza tasnia hiyo.
    "Katika Hotuba ya Mhe.Rais wa Jamhuri ya Muungano wa  Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli wakati wa ufunguzi wa Bunge ya  alieleza azma ya Serikali kuendeleza tasnia ya Sanaa, hivyo basi ni jukumu lenu kama wadau kutoa ushauri wa nini kifanyike ili kuendeleza tasnia yenu kwani Serikali ya awamu ya tano inataka kuacha alama katika sekta ya sanaa," alisema Dkt. Abbasi.



    Akiendelea kuzungumza katika kikao hicho cha wadau hao ambacho ni sehemu ya ziara yake ya kukutana na makundi mbalimbali ya Sanaa  Dkt.Abbasi aliwasihi wasanii hao wa kutoa hoja kwani wao ndiyo wanaofahamu kwa undani changamoto zinazokwamisha mafanikio katika uendeshaji wa shughuli za muziki nchini. 
    "Serikali hii ya Awamu ya Tano inawathamini sana Wasanii na itaendelea kufanya kazi nanyi kwa pamoja ila ni lazima nanyi mjithamini na kuwa wazalendo," alisema Dkt.Abbasi.
    Pamoja na hayo Katika Mkuu huyo na Msemaji Mkuu wa Serikali aliwasisitiza wasanii hao kuacha kuwa na maugomvi na kuzingatia maadili.
    Akizungumza kuhusu mikakati ya Serikali katika kuendeleza  tasnia ya Sanaa Dkt.Abbasi alisema kuwa tayari wamempatia mtaalamu wa kuchora ramani ya kisasa ya Jengo la "Arts Arena" ambalo litakuwa la kisasa na litasaidia kufanya shughuli za Sanaa ikiwemo matamasha makubwa.
    Pamoja na hayo naye Katibu Mtendaji Taasisi  ya Hakimiliki na Hakishiriki  (COSOTA) Doreen Sinare alieleza serikali katika kupambana na masuala ya uharamia wa kazi za wasanii imeongeza  malipo ya faini na kufikia zaidi ya milioni ishirini, pia kuna maboresho mbalimbali yamefanyika katika Kanuni kwa ajili ya kuongeza wigo wa ukusanyaji mirabaha ya kazi za wasanii.
    Halikadhalika nae Msanii wa HipPop  Niki wa Pili alitoa maoni kwa Serikali kuangalia namna ya kutafuta mzawa ambaye atashughulikia usimamizi wa ukusanyaji wa wasambazaji na mauzo ya nyimbo za wasanii katika "digital platform" ili kuweza kumsaidia msanii kunufaika na kazi yake kwa wakati.
    Hata hivyo nae mmoja wa Wasanii Bongo Fleva Msami Jovian alitoa ombi kwa Serikali kuangalia Online TV kwani zimekuwa zikitumika kutangaza mambo yasiyo na maadili kwa ajili ya kutoa "kiki".
    Akihitimisha mkutano huo Dkt.Abbasi aliwaeleza wasanii hao kuwa tayari Mfuko wa Maendeleo ya Sanaa na Utamaduni upo tayari na wajumbe wa bodi yake tayari wameshateuliwa, na unatarajiwa kuzinduliwa mara baada ya uteuzi wa Waziri wa wizara hiyo.
    Pia alisema mapema mwanzoni mwa mwaka ujao wizara yake itaandaa tuzo kwa ajili ya wasanii kwa lengo la kutoa motisha kwa kazi wanazozifanya pamoja na kutoa fursa kwa wasanii kuwa wabunifu zaidi.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: WIZARA YAWATAKA WASANII WA BONGO FLEVA KUWASILISHA SERIKALINI MAHITAJI YA KUBORESHA TASNIA YA MUZIKI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top