• HABARI MPYA

  Wednesday, December 23, 2020

  MHE.BASHUNGWA ASEMA SERIKALI ITAENDELA KUSHIRIKIANA NA TFF KUENDELEZA MICHEZO

  Na Shamimu Nyaki – WHUSM, Dar es Salaam
  WAZIRI wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Innocent Bashungwa ameliagiza Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kuweka kipaumbele kwenye michezo ya watoto wa shule za msingi na sekondari ili kupata wachezaji wazuri wa baadaye kwa ajili ya timu za taifa.
  Waziri Bashungwa ameyasema hayo leo Jijini Dar es Salaam alipofanya kikao na viongozi wa TFF kwa pamoja na Naibu wake, Abdallah Ulega.
  Waziri Bashungwa amesema lazima TFF Serikali na TFF wawe na Mpango Mkakati wa pamoja wa kuendesha michezo nchini.
  "Nasisitiza utawala bora katika kuendesha michezo ikiwemo usimamizi madhubuti wa fedha zinazoingia TFF" alisema Waziri Bashungwa.


  Amesema Serikali imetenga shule 56 kwa ajili ya kufundisha michezo lengo ni kuzalisha wanamichezo wengi na bira nchini.
  "Serikali tuko tayari kushirikiana na TFF, Hivyo lazima shughuli zote za michezo za timu za taifa za ndani na nje ya nchi Serikali iwe na taarifa" Waziri Mhe.Bashungwa.
  Kwa upande wake Naibu Waziri wa wizara hiyo Mhe. Abdallah Ulega amesisitiza kuwa Shirikisho hilo lisimamie mchango wa soka katika kupata fedha za kuhudumia timu za Taifa. 
  "Ni lazima tuzo kwa wanamichezo zirejee na zipewe uzito unaostahili, lengo ni kutambua mchango wa wanamichezo katika Taifa letu" alisema Naibu Waziri Ulega
  Naibu Waziri Ulega amesisitiza kuwa TFF isimamie vilabu vinavyoshiriki Kombe la Mapinduzi kupeleka timu bora kwa heshima ya kombe hilo.
  Naibu Waziri amesisitiza pia uhamasishaji wa michezo kwa timu za Taifa ikiwemo   uhamisishaji wa ununuzi wa jezi za timu ya Taifa.
  Naye, Rais wa TFF, Wallace Karia amesema kwamba Shirikisho lao limeanza kutekeleza Ilani ikiwemo kuwa na Mpango Mkakati wa kuendeleza michezo pamoja na kuimarisha Utawala Bora.
  Vilevile, Katibu Mkuu wa Shirikisho hilo Bw.Alfred Kidau ameeleza kuwa maandaalizi ya kushiriki Kombe la CHAN yameanza ambapo timu zitaingia kambini Januari 2021.
  Katika Hatua nyingine, Waziri Bashungwa amesisitiza kuwa Michezo itaendelea kuwa nyenzo katika kudumisha Muungano. Amesema hayo leo pia Jijini Dar es Salaam katika Kikao cha Maandalizi ya kushiriki Michezo ya Olimpiki Tokyo mwaka 2021.
  Akiendelea kuzungumza katika Kikao hicho kilichoshirikisha Baraza la Michezo la Taifa, Baraza la Michezo Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Kamati ya Maandalizi ya Olimpiki, Chama cha Riadha pamoja na Shirikisho la ngumi alisema kikao hicho kinalenga kujadili namna Taifa hili litakavyoshiriki Michezo hiyo.
  "Naendelea kusisitiza suala la Utawala Bora kwa Vyama na Mashirikisho yote ya Michezo, pia hakikisheni mnasaidia ustawi wa timu zetu za Taifa,"alisema, Mhe.Bashungwa.
  Aidha, Mhe.Bashungwa aliagiza kuwa Maazimio yote ya kikao hicho yafanyiwe kazi, ikiwemo maandalizi ya kutosha ya Michezo ya Kimataifa pamoja na uwezo wanamichezo wanaoshiriki mashindano hayo. 
  Kwa upande wa Naibu Waziri wa Wizara hiyo Mhe. Abdallah Ulega amevitaka Vyama na Mashirikisho ya Michezo kuwa na vipaumbele katika michezo, ambapo amesisitiza kuwa lazima nchi kuwa na michezo ya vipaumbele ambayo itafanya vizuri ndani na nje ya nchi.
  "Sisi wasimamizi wa Sekta ya Michezo Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar tutasimamia maono ya Marais wetu katika kukuza na kuendeleleza Sekta hizi," alisema, Mhe.Ulega.
  Naye Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Dkt. Hassan Abbasi ameeleza kuwa dhamira ya Serikali ni kulifikisha Taifa hili linapostahili katika sekta ya michezo, huku akisistiza kuwa suala la kuwa na chanzo cha kuaminika katika kuendesha michezo Serikali inaendelea kulisimamia.
  Vilevile, Mwanariadha wa zamani Selemani Nyambui ameipongeza Serikali kwa dhamira yake ya kukuza michezo ambapo amesema kuwa sekta hiyo ni muhimu katika ustawi wa vijana wenye vipaji na ari ya kuisaidia nchi kupitia michezo.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: MHE.BASHUNGWA ASEMA SERIKALI ITAENDELA KUSHIRIKIANA NA TFF KUENDELEZA MICHEZO Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top