• HABARI MPYA

  Wednesday, December 16, 2020

  WAZIRI BASHUNGWA AIAGIZA KAMATI YA KUSIMAMIA HAKI ZA WASANII KULETA MATOKEO CHANYA

  Na Shamimu Nyaki – WHUSM, DAR ES SALAAM
  WAZIRI wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Innocent Bashungwa ametoa agizo kwa  Bodi ya Filamu  Tanzania  kuhakikisha  Kamati ya kusimamia Haki za Wasanii inafanya kazi hiyo kwa weledi na kasi kwa ajili ya maslahi ya wasanii.
  Mhe Bashungwa ametoa agizo hilo   Desemba 15, 2020 alipotembelea Bodi ya Filamu   Tanzania akiwa pamoja na Naibu wake Abdallah Ulega pamoja na Katibu Mkuu Dk. Hassan Abbasi ambapo ameitaka Kamati hiyo kuwasilisha serikalini Mpango mkakati wa namna inavyotekeleza jukumu hilo.
  “Naiagiza Bodi ya Filamu nchini kuhakikisha maudhui na maadili ya filamu zinazotengezwa nchini zinakuwa bora ambazo zitaleta ushindani katika soko ndani na nje ya nchi, lakini pia lazima zizingatie utamaduni wa nchi yetu”,alisema Mhe.Bashungwa.


  Waziri wa Habari, Utamaduni Sanaa na Michezo Mhe. Innocent Bashungwa akizungumza na watendaji wa Bodi ya Filamu Tanzania alipotembelea Taasisi hiyo 

  Aidha Waziri huyo ameongeza kuwa atahakikisha Bodi ya Filamu, BASATA na COSOTA zinakua katika jengo moja kwakua wadau wake ni wa aina moja, lengo ni kurahisisha huduma kwa wadau hao ambao wamekua na mchango mkubwa katika kukuza pato la taifa na kuongeza ajira.
  Kwa upande wake Naibu Waziri wa wizara hiyo Mhe. Abdallah Ulega amewapongeza wasanii wote nchini kwa kufanya kazi nzuri  ambayo inawaingizia kipato na kuitangaza nchi vizuri  pamoja na kukuza uchumi wa nchi, ambapo amesema mafanikio hayo yametokana na Sera nzuri ziliowekwa na Serikali kwa ajili ya kundi hilo, huku ankinukuu maneno ya Mhe. Waziri Bashungwa kuwa “msanii kichwa chake ndio kiwanda chake”.
  Mhe.Ulega ameongeza kuwa Kamati inayosimamia Haki za Wasanii ifuatilie haki zote za wasanii ambao wameshatangulia mbele za haki kama marehemu Steven Kanumba na wengineo ili ziwanufaishe wanaohusika na marehemu hao. 
  “Nawaagiza Maafisa Utamaduni nchini kutekeleza majukumu  yao kwa weledi mkubwa kwakua ndio daraja la kuratibu na kusimamia kazi za sanaa kuanzia ngazi ya chini, hivyo ni jukumu lao kuhakikisha kazi za Sanaa na wasanii zinaratibiwa kwa kufuata mwongozo wa Bodi ya Filamu, BASATA na COSOTA pamoja na matwaka ya  Sera ya Utamaduni ya mwaka 1997”,alisema Mhe.Ulega

  Waziri Innocent Bashungwa (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na Naibu wake, Abdallah Ulega na Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Dk. Hassan Abbasi, pamoja na watendaji wa Bodi ya Filamu Tanzania

  Naye Katibu Mkuu wa wizara hiyo Dkt. Hassan Abbasi amesema Taasisi hiyo imefanya mageuzi ya kiutendaji ikiwemo kuhuisha muundo kiutumishi kwakua ni taasisi mojawapo yenye dhamana madhubuti kwa wadau wake, huku aisisitiza kuwa Bodi hiyo itaendelea kufanya vizuri katika majukumu yake.
  Hata hivyo Katibu Mtendaji wa Bodi ya Filamu Dkt. Kiango Kilonzo ameeleza mafanikio ambayo bodi imepata kuwa ni pamoja na kuonyesha filamu za kitanzania katika chaneli ya Maisha Magic Bongo ya DSTV, kusimamia chaguzi za vyama na mashirikisho ya filamu nchini, pamoja ni kupata  Tuzo 200 za kitaifa kwa wadau wa filamu.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: WAZIRI BASHUNGWA AIAGIZA KAMATI YA KUSIMAMIA HAKI ZA WASANII KULETA MATOKEO CHANYA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top