• HABARI MPYA

  Wednesday, December 23, 2020

  YANGA SC YAITANDIKA IHEFU SC 3-0 NA KUKAMILISHA MZUNGUKO WA KWANZA LIGI KUU BILA KUPOTEZA MECHI

  VIGOGO, Yanga SC wamekamilisha mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara bila kupoteza mechi kufuatia ushindi wa 3-0 dhidi ya Ihefu SC jioni ya leo Uwanja wa Sokoine Jijini Mbeya.
  Kwa ushindi huo, Yanga SC inayofundishwa na kocha Mrundi, Cedric Kaze inafikisha pointi 43 baada ya mechi 17 za duru la kwanza, ikiendelea kuongoza Ligi Kuu kwa pointi 11 zaidi ya mabingwa watetezi, Simba SC ambao hata hivyo wana mechi tatu mkononi.
  Katika mchezo wa leo uliochezeshwa na refa Hussein Athumani wa Katavi aliyesaidiwa na Jesse Erasmo wa Morogoro na Abdallah Rashid wa Pwani, hadi mapumziko Yanga SC walikuwa mbele kwa bao 1-0.
  Bao hilo limefungwa na kiungo mzawa, Deus David Kaseke dakika ya 12 akimalizia kazi nzuri ya kiungo mpya, Mrundi Said Ntibanzokiza.
  Ntibanzokiza, mchezaji wa zamani wa NEC ya Uholanzi, Cracovia ya Poland, Akhisar Belediyespor ya Uturuki, Caen ya Ufaransa, FC Kaysar ya Kazakhtan na Vital’O ya kwao, Burundi akamsetia mshambuliaji Mburkinabe, Yacouba Songne kufunga bao la pili dakika ya 49.
  Kocha Kaze akampumzisha Mrundi mwenzake huyo aliyesajiliwa dirisha dogo, mwezi huu na kumuingiza kiungo wa zamani wa Teneriffe ya Hispania, Farid Mussa na Yanga ikapata bao la tatu lililofungwa na kiungo mwingine mzawa, Feisal Salum dakika ya 60 akimalizia pasi ya Kaseke.
  Mechi nyingine za Ligi Kuu leo, bao pekee la Seif Abdallah Karihe dakika ya tatu limeipa Dodoma Jiji FC ushindi wa 1-0 dhidi ya wenyeji, Mtibwa Sugar Uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro.
  Na mabao ya mshambuliaji wa zamani wa Simba SC na Azam FC, Daniel Lyanga dakika ya 52 na 74 yakaipa JKT Tanzania ushindi wa 2-0 dhidi ya KMC Uwanja wa Jamhuri mjini Dodoma.
  Kikosi cha Ihefu SC kilikuwa; Deogratius Munishi ‘Dida’, Mando Mkumbwa, Omary Kindamba, Wema Sadoki, Michael Masinda, Samuel Jackson, Juma Mahadhi/Andrew Simchimba dk68, Jeremiah Katula/ Omary Hamis dk43, Joseph Kinyozi, Shaaban Iddi/Godfrey Kitenga dk49 na Joseph Mahundi.
  Yanga SC; Metacha Mnata, Kibwana Shomary, Yassin Mustapha, Lamine Moro, Bakari Mwamnyeto, Mukoko Tonombe/Zawadi Mauya dk46, Tuisila Kisinda, Feisal Salum, Deus Kaseke/Haruna Niyonzima dk77, Yacouba Sogne na Said Ntibanzokiza/Farid Mussa dk58.

  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: YANGA SC YAITANDIKA IHEFU SC 3-0 NA KUKAMILISHA MZUNGUKO WA KWANZA LIGI KUU BILA KUPOTEZA MECHI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top