• HABARI MPYA

  Alhamisi, Julai 23, 2020

  SERGE WAWA PASCAL ATOLEWA KWA KADI NYEKUNDU SIMBA SC YATOKA SULUHU NA COASTAL UNION MKWAKWANI

  Na Mwandishi Wetu, TANGA
  PAMOJA na kucheza pungufu kwa robo saa yote ya mwisho ya mchezo, lakini mabingwa, Simba SC wamefanikiwa kulazimisha sare ya bila kufungana na wenyeji, Coastal Union katika mchezo wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara jioni ya leo Uwanja wa Mkwakwani Jijini Tanga.
  Beki tegemeo na nguzo ya mafanikio ya mataji matatu mfululizo ya ubingwa wa Ligi Kuu kwA Wekundu hao wa Msimbazi, Muivory Coast, Serge Pascal Wawa alitolewa kwa kadi nyekundu dakika ya 75 baada ya kuonyesha utovu wa nidhamu mbele ya refa Ludovic Charles wa Mwanza.
  Wawa, beki wa zamani wa Azam FC na El-Merreikh ya Sudan alitolewa baada ya kuudunda mpira chini kwa hasira kuashiria kukerwa na maamuzi ya refa kufuatia awali kuonyeshwa kadi ya njano kwa kucheza rafu dakika ya 69.

  Hata hivyo, mabingwa mara 21 wa Ligi Kuu wakafanikiwa kumalizia mchezo wao wa 37 wa msimu bila kuruhusu bao, hivyo kufikisha pointi 85, sasa wakiwazidi pointi  16 watani wao wa jadi, Yanga SC wanaofuatia nafasi ya pili.
  Mechi nyingine za Ligi Kuu leo, bao pekee la Daruwesh Saliboko kwa penalty dakika ya 78 limeipa ushindi wa 1-0 Lipuli FC dhidi ya Ruvu Shooting Uwanja wa Samora mjini Iringa.
  Uwanja wa Ushirika mjini Moshi mkoani Kilimanjaro, Edward Songo akaifungia bao la kusawazisha JKT Tanzania dakika ya 50 ikitoa sare ya 1-1 na wenyeji, Polisi Tanzania waliotangulia kwa bao la Matheo Anthony dakika ya 32.
  Alliance FC ikalazimishwa sare ya 2-2 na Ndanda SC kutoka Mtwara. Mabao ya Alliance yamefungwa na Israel Patrick dakika ya tisa na Martin Kiggi dakika ya 60, wakati ya Ndanda SC yamefungwa ya Abdul Khamis dakika ya 16 na Omary Mponda dakika ya 51.
  Mchezo mwingine wa Ligi Kuu unaendelea hivi sasa kati ya wenyeji, Azam FC na Mbeya City Uwanja wa Azam Complex, Chamazi nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam.
  Kikosi cha Coastal Union kilikuwa; Abubakar Ibrahim, Hassan Kibailo, Hance Masoud, Bakari Mwamnyeto, Ibrahim Ame, Salum Ally, Mtenje Albano, Ayoub Lyanga, Mudathir Abdallah/Shaaban Iddi dk83, Ayoub Semtawa na Issa Abushehe.
  Simba SC; Beno Kakolanya, Shomari Kapombe, Mohamed Hussein ‘Tshabalala’, Erasto Nyoni, Pascal Wawa, Jonas Mkude, Hassan Dilunga, Muzamil Yassin, Meddie Kagere, John Bocco/Clatous Chama dk69 na Miraj Athumani ‘Madenge’/Deo Kanda dk69. 
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: SERGE WAWA PASCAL ATOLEWA KWA KADI NYEKUNDU SIMBA SC YATOKA SULUHU NA COASTAL UNION MKWAKWANI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top