• HABARI MPYA

    Sunday, July 26, 2020

    ALLIANCE FC, NDANDA SC, LIPULI FC ZAUNGANA NA SINGIDA UNITED KUSHUKA DARAJA LIGI KUU

    Na Mwandishi Wetu, MWANZA
    TIMU za Alliance FC ya Mwanza, Ndanda SC ya Mtwara na Lipuli FC ya Iringa zimeungana na Singida United kushuka daraja baada ya mechi za mwisho za Ligi Kuu ya Tanzania Bara leo.
    Alliance FC imeshuka licha ya ushindi wa 3-2 dhidi ya Namungo FC Uwanja wa Nyamagana Jijini Mwanza. 
    Mabao ya Alliance FC yamefungwa na Martin Kiggi dakika ya kwanza, Israel Patrick dakika ya 25 na Juma Nyangi dakika ya 65, wakati ya Namungo FC yamefungwa na Bigirimana Blaise dakika ya nane na Frank Mkumbo dakika ya 61.
    Ndanda SC yenyewe imechapwa 2-0 na Mbao FC, mabao ya Jordan John dakika ya 66 na Waziri Junior dakika ya 18 Uwanja wa CCM Kirumba mjini Mwanza, wakati Lipuli imechapwa 1-0 na Yanga SC, bao pekee la David Molinga dakika ya 38 Uwanja wa Samora mjini Iringa.
    Alliance FC ya Mwanza imeungana na Ndanda SC ya Mtwara, Lipuli FC ya Iringa na Singida United kushuka daraja 




    Mechi nyingine za Ligi Kuu leo, Simba SC imeshinda 2-1 dhidi ya Polisi Tanzania Uwanja wa Ushirika mjini Moshi mkoani Kilimanjaro. Mabao ya Simba SC yamefungwa yote leo yamefungwa na Nahodha wake, John Raphael Bocco dakika ya pili na 45 na ushei, wakati la Polisi limefungwa na Marcel Kaheza dakika ya 30.
    Tanzania Prisons imelazimishwa sare ya 2-2 na Azam FC Uwanja wa Sokoine mjini Mbeya. Mabao ya Prisons yamefungwa na Abdallah Kheri aliyejifunga dakika ya 11 na Vedastus Mwihambi dakika ya 39, wakati ya Azam FC yamefungwa na Jumanne Elifadhili aliyejifunga dakika ya kwanza na Never Tigere dakika ya 59.
    Nayo Mtibwa Sugar ikaichapa 2-1 Ruvu Shooting mabao yake yakifungwa na Boban Zilintusa dakika ya 51 na 65 la wageni likifungwa na Saadat Mohamed dakika ya 35.
    Mbeya City wakaibuka na ushindi wa 3-0 ugenini dhidi ya KMC Uwanja wa Azam Complex, Chamazi Jijini Dar es Salaam mabao ya Rehani Kibingu dakika ya 68, Abasarim Chidiebele dakika ya 87 na Peter Mapunda dakika ya 90 na ushei kwa penalti.
    Bao pekee la Najim Magulu dakika ya 79 likawapa JKT Tanzania ushindi wa ugenini wa 1-0 dhidi ya Coastal Union Uwanja wa Mkwakwani, Tanga.
    Mwadui FC wakaichapa Kagera Sugar 2-1 Uwanja wa Mwadui Complex, Kishapu mkoani Shinyanga. Mabao ya Mwadui FC yamefungwa na Wallace Kiango dakika ya 13 na 17 kwa penalti wakati la Kagera Sugar limefungwa na Nasoro Kapama dakika ya 68.
    Biashara United ikaichapa 2-0 Singida United Uwanja wa Liti mjini Singida, mabao ya Deogratius dakika ya 20 na David Nartey aliyejifunga dakika ya 27.
    Mbao na FC ya Mwanza na Mbeya City zitakwenda kucheza mechi za mchujo dhidi ya timu za Daraja la Kwanza kuwania kubaki Ligi Kuu.
    Mbao FC itamenyana na Ihefu SC Uwanja wa Highlands Estates, Mbarali mkoani Mbeya na Geita Gold itamenyana na Mbeya City Uwanja wa sekondari ya Nyankumbu, Geita Julai 29.
    Timu hizo zitarudiana Agosti 1, Mbao FC wakiwaalika Ihefu Uwanja wa CCM Kirumba na Mbeya City wakiwa wenyeji wa Geita Gold Uwanja wa Sokoine.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: ALLIANCE FC, NDANDA SC, LIPULI FC ZAUNGANA NA SINGIDA UNITED KUSHUKA DARAJA LIGI KUU Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top