• HABARI MPYA

  Jumatano, Julai 08, 2020

  AZAM FC YAICHAPA MWADUI 1-0 CHAMAZI NA KUREJEA KWENYE NAFASI YA PILI LIGI KUU

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  TIMU ya Azam FC imeutumia vyema Uwanja wa nyumbani baada ya ushindi wa 1-0 dhidi ya Mwadui FC ya Shinyanga kwenye mchezo wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara usiku wa leo.
  Pongezi kwa mfungaji wa bao hilo pekee, Andrew Simchimba dakika ya 70 akiunganisha kwa guu la kushoto krosi maridadi ya kiungo Salum Abubakar ‘Sure Boy’ kutoka upande wa kulia.
  Kwa ushindi huo, Azam FC inafikisha pointi 65 na kurejea nafasi ya pili sasa ikiwazidi vigogo, Yanga SC pointi moja na wote wakiwa nyuma ya mabingwa tayari kwa mara ya tatu mfululizo, Simba SC wenye pointi 81 baada ya wote kucheza mechi 34.  Mechi nyingine za leo, Simba SC wamelazimishwa sare ya bila kufungana na wenyeji, Namungo FC Uwanja wa Majaliwa, Ruangwa mkoani Lindi, huku watani wao, Yanga SC wakiibuka na ushindi wa 1-0 dhidi ya Kagera Sugar Uwanja wa Kaitaba, Bukoba, bao pekee la Bernard Morrison dakika ya 78.
  KMC imeshinda 2-0 dhidi ya Singida United, mabao ya Charles Ilanfya dakika ya 39 na Mohamed Samatta dakika ya 85 Uwanja wa Azam Complex, wakati bao pekee la Waziri Junior dakika ya 64 limeipa Mbao FC ushindi wa 1-0 dhidi ya Mtibwa Sugar Uwanja wa CCM Kirumba Jijini Mwanza.
  Uwanja wa Karume mjini Musoma mkoani Mara, wenyeji Biashara United wamelazimishwa sare ya 0-0 na Ruvu Shooting na Uwanja wa Nangwanda Sijaona mjini Mtwara, Ndanda SC pia wametopa sare ya 0-0 na JKT Tanzania.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: AZAM FC YAICHAPA MWADUI 1-0 CHAMAZI NA KUREJEA KWENYE NAFASI YA PILI LIGI KUU Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top