• HABARI MPYA

  Tuesday, July 28, 2020

  RAIS DK. MAGUFULI AUBADILI JINA UWANJA WA TAIFA, SASA KUITWA UWANJA WA MKAPA

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. John Pombe Joseph Magufuli ameubadili jina Uwanja wa Taifa na sasa utakuwa unajulikana kama Uwanja wa Mkapa ili kumuenzi Rais mstaafu wa Serikali ya awamu ya tatu nchini, marehemu Dk. Benjamin William Mkapa.
  Mkapa aliyefariki dunia Julai 24 Jijini Dar es Salaam ndiye aliyefanikisha ujenzi wa Uwanja huo wa kisasa wa michezo nchini.
  Akizungumza wakati wa zoezi la kuuaga na kutoa heshima za mwisho kwa mwili wa marehemu Mkapa uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam leo, Rais Dk. Magufuli amesema kwamba Watanzania hawatamsahau Rais huyo mstaafu wa awamu ya tatu kwa kuwaachia Uwanja huo.
  Rais Dk. John Pombe Joseph Magufuli ameubadili jina Uwanja wa Taifa na sasa utakuwa unajulikana kama Uwanja wa Mkapa aliyefariki dunia Julai 24 Jijini Dar es Salaam 

  “Najua Watanzania hawatamsahau Mzee Mkapa kwa kuwajengea Uwanja mkubwa wa michezo tunaouona mbele yetu. Kwa sasa wengi wanataka Uwanja ule uitwe Uwanja wa Mkapa au Mkapa Stadium,”. 
  “Ninajua Mzee Mkapa hakupenda sana vitu viitwe kwa jina lake, lakini kwa sababu meseji nimezipata nyingi na kwa sababu sasa hawezi akaniadhibu chochote, yeye amelala hapo basi natamka Uwanja huo utaitwa Mkapa Stadium ili tuweze kumuenzi na kumkumbuka kwa kazi kubwa aliyoifanya kwa ajili ya kuendeleza maslahi ya michezo katika taifa letu,”amesema Rais Dk Magufuli. 
  Pamoja na hayo, Dk Magufuli amesema kwamba anasikia marehemu Mkapa alikuwa mpenzi wa klabu kongwe nchini, Yanga SC kama ilivyo Rais wa Mstaafu wa Awamu ya Nne, Jakaya Mrisho Kikwete, ingawa pia alisema hafahamu Rais Mstaafu wa Awamu ya Pili, Ali Hassan Mwinyi hafahamu ni timu gani..
  “Hata kwenye michezo na sanaa, alitoa mchango, tena nasikia alikuwa ni mshabiki mkubwa wa Yanga, ingawa sikuwahi kumsikia akisema hilo hadharani. Mzee Kikwete hapa anasema ni kweli kwa sababu hata Kikwete na yeye ni Yanga, sifahamu Mzee Mwinyi yeye ni timu gani,”alisema Dk Magufuli.
  Mwili wa marehemu Mzee Mkapa umeagwa leo Uwanja wa Uhuru kabla ya kusafirishwa kwenda kijijini kwake Lupaso ambako atazikwa kesho saa nane mchana. 
  Mzee Mkapa alizaliwa Novemba 12 mwaka 1938, kijiji cha Ndanda, jirani na Masasi mkoani Mtwara na alikuwa Rais wa kwanza wa Tanzania baada ya demokrasia ya Vyama Vingi vya siasa kuanzia mwaka 1995 hadi 2005.
  Wanamichezo nchini watamkumbuka daima Mzee Mkapa kutokana na kuwaachia Uwanja mzuri wa kisasa wa michezo – Taifa uliopo Dar es Salaam.
  Wakati anafunga Michezo ya UMISETA mwaka 2000, Rais Mkapa alitoa ahadi ya kuwaachia watanzania Uwanja mzuri wa kisasa michezo kabla ya kumalza muda wake mwaka 2005 – lakini ulifunguliwa mwaka 2007.   Mungu ampumzishe kwa amani Rais Mstaafu wa awamu ya tatu, Ben Mkapa.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: RAIS DK. MAGUFULI AUBADILI JINA UWANJA WA TAIFA, SASA KUITWA UWANJA WA MKAPA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top