• HABARI MPYA

  Jumamosi, Julai 11, 2020

  SIMBA WALIVYOFURAHIA UBINGWA WA TATU MFULULIZO WA LIGI KUU

  Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
  MASHABIKI wa Simba walijitokeza kwa wingi Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam (JNIA) mapema Julai 9, mwaka 2020 kuwapokea mashujaa wao wakitokea Ruangwa mkoani Lindi, ambako ambako siku iliyotangulia walikabidhiwa Kombe la ubingwa wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara.
  Simba SC ilikabidhiwa Kombe hilo baada ya mechii dhidi ya wenyeji, Namungo FC iliyomalizika kwa sare ya bila kufungana Uwanja wa Majaliwa, hivyo kufikisha pointi 81 baada ya kucheza mechi 34 ambazo haziwezi kufikiwa na wapinzani.
  Mechi dhidi ya Tanzania Prisons Uwanja wa Sokoine Jijini Mbeya iliyomalizika kwa sare ya 0-0 ndiyo iliyoihakikishia Simba ubingwa baada ya kufikisha pointi 79 katika mchezo wa 31 ambazo haziwezi kufikiwa pia na timu nyingine yoyote ya Ligi Kuu.
  Simba inatwaa ubingwa wa Ligi Kuu kwa mara ya tatu mfululizo ikiwa imebakiza mechi tano – huku wakiwaacha watani wao wa jadi, Yanga wakiwania nafasi ya pili dhidi ya Azam FC na Namungo FC.
  Hilo linakuwa taji la 21 la Ligi Kuu kwa Simba SC baada ya awali kulibeba katika misimu ya 1965, 1966, 1973, 1976, 1977, 1978, 1979, 1980, 1984, 1990, 1994, 1995, 2001, 2003, 2004, 2007, 2010, 2012, 2018 na 2019.
  Lakini hii ni mara ya pili tu Simba inatwaa taji la Ligi Kuu zaidi ya mara mbili mfululizo, baada ya awali kulibeba mara tano mfululizo kuanzia 1976 hadi 1980.

  Na ndiyo kipindi hiki Simba iliwapa kipigo cha kihistoria watani wao wa jadi, Yanga cha 6-0 Julai 19, 1977, Abdallah Athumani Seif, maarufu Abdallah Kibadeni akiweka rekodi ya mchezaji pekee kufunga hat trick kwenye mechi za watani, mabao mengine yakifungwa Jumanne Hassan 'Masimenti' mawili na Suleiman Sanga aliyejifunga.
  Vigogo, Yanga SC wanabaki kuwa mabingwa mara nyingi zaidi wa taji hilo, 27 katika misimu ya 1968, 1969, 1970, 1971, 1972, 1974, 1981, 1983, 1985, 1987, 1989, 1991, 1992, 1993, 1996, 1997, 1998, 2002, 2005, 2006, 2008, 2009, 2011, 2013, 2015, 2016 na 2017.


  Timu nyingine zilizobeba taji hilo ni Cosmopolitans ya Dar es Salaam 1967, Mseto SC ya Morogoro 1975, Pan African ya Dar es Salaam 1982, Tukuyu Stars ya Mbeya 1986, Coastal Union ya Tanga 1988, Mtibwa Sugar ya Morogoro 1999 na 2000 na Azam FC 2014.
  Uongozi madhubuti chini ya Mwenyekiti wa Bodi, Mohamed ‘Mo’ Dewji uliounda kikosi imara na benchi madhubuti la Ufundi chini ya kocha Mbelgiji, Sven-Ludwig Vandenbroeck ndiyo siri ya mafanikio ya Wekundu wa Msimbazi kwa misimu hii mitatu mfululizo.
  Mfumo mzuri wa uendeshwaji wa klabu kwa sasa chini ya Mtendaji Mkuu, Senzo Mazingisa Mbatha raia wa Afrika Kusini unawapa Simba SC kiburi cha kuamini wanaweza kuendelea kutwaa taji hilo kwa miaka mingine saba.
  Hongera Simba Sports Club kwa mafaniko hayo.   • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: SIMBA WALIVYOFURAHIA UBINGWA WA TATU MFULULIZO WA LIGI KUU Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top