• HABARI MPYA

  Ijumaa, Julai 03, 2020

  BODI YA LIGI YAWAONYA MBEYA KURUHUSU MASHABIKI KUVAMIA UWANJANI SOKOINE BAADA YA MECHI

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  KAMATI ya Uendeshaji na Usimamizi wa Ligi ya Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB) imetoa Onyo kali kwa Uwanja wa Sokoine, Chama cha Soka Mbeya na klabu zote zinazotumia uwanja wa Sokoine kama uwanja wa nyumbani kwa kosa la mashabiki kuingia uwanjani baada ya mchezo kumalizika.
  Kamati inawataka Chama cha Soka wa Mbeya, wamiliki wa uwanja wa Sokoine na klabu zote zinazotumia uwanja wa Sokoine kuhakikisha zinazingatia kanuni ya 14(10), 14(11),14(42) na 14(43) inayohusu taratibu za mchezo inayosema:-
   “Ni marufuku kwa viongozi kuingia uwanjani(pitch) bila sababu za msingi kinyume na taratibu za mchezo kabla, wakati au baada ya mchezo”.
  “Ni marufuku kwa mashabiki kuingia uwanjani kabla,wakati au baada ya mchezo”.
   “Katika mchezo wowote wa ligi kuu wakati mchezo ukiwa unachezwa hairuhusiwi kufanyika shughuli nyingine yoyote katika uwanja wa kuchezea na eneo la uwanja wa ndani ya uzio wa ndani wa uwanja kama vile muziki, ujenzi na kuendeshwa kwa vyombo vya moto na visivyo vya moto”
  “Hairuhusiwi kwa viongozi wa klabu, mashabiki na mtu yeyote asiyekuwa na kazi maalum kuhusiana na mchezo katika eneo la uwanja(pitch) kuwepo eneo la uwanjani ndani kuzunguka uwanja wa kuchezea(pitch)”.
  Kamati inatoa Onyo na angalizo kuwa kanuni hizo zisipozingatiwa uwanja huo utafungiwa mara moja.
  Nayo KMC FC imepigwa faini ya Sh. 500,000 kwa kosa la wachezaji wake watano kuonyeshwa kadi za njano sita na nyekundu moja katika mechi dhidi ya Kagera Sugar iliyomalizika kwa sare ya 1-1 Juni 28 Uwanja wa Kaitaba na adhabu hiyo imetolewa kwa kujibu wa kanuni ya 43(10) kuhusu udhibiti wa klabu.
  Nayo Dodoma FC imepigwa faini ya Sh. 200,000 kwa kosa la kugoma kuingia vyumbani baada ya kukuta yai limepasuliwa mbele ya lango la kuingilia katika chumba chao cha kubadilishia na kusababisha zoezi la ukaguzi wa wachezaji lifanyike nje ya chumba katika mchezo uliochezwa Juni 27, 2020 mkoani Ruvuma.
  Adhabu hii imetolewa kwa uzingativu wa kanuni ya 14(49) ya ligi daraja la kwanza kuhusu Taratibu za mchezo.
  Kiongozi wa timu ya Ruvuma Queens Bw. Issa Telela amepelekwa kamati ya nidhamu ya TFF kwa kosa la kumtemea mate mwamuzi wa akiba katika mchezo uliochezwa Juni 27, 2020 kwenye uwanja wa Sokoine Mkoani Ruvuma.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: BODI YA LIGI YAWAONYA MBEYA KURUHUSU MASHABIKI KUVAMIA UWANJANI SOKOINE BAADA YA MECHI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top