• HABARI MPYA

  Ijumaa, Juni 29, 2018

  AZAM FC YAANZA VYEMA KOMBE LA KAGAME, YAICHAPA KATOR FC 2-1 MABAO YOTE KAFUNGA SHAABAN IDD CHILUNDA

  Na Sada Salmin, DAR ES SALAAM
  MABINGWA watetezi wa Kombe la Kagame, Azam FC wameanza vizuri harakati za kutetea ubingwa wao baada ya jioni ya leo kuifunga Kator FC ya Sudan Kusini mabao 2-1 katika mchezo wake wa kwanza wa michuano hiyo.
  Katika mchezo huo uliochezwa kuanzia saa 11:00 jioni kwenye Uwanja wa Azam Complex uliopo Chamazi Mbagala jijini Dar es Salaam, mabao mawili ya Azam FC yalifungwa na mshambuliaji Shaaban Idd Chilunda.
  Chilunda aliifungia Azam FC bao la kwanza katika dakika ya 28, bao lililodumu hadi mapumziko na katika kipindi cha pili dakika ya 48 Chilunda alifunga bao la pili akipokea pasi ya Bruce Kangwa.

  Kator FC yenye wachezaji mchanganyiko kutoka Uganda na Kenya, ilipata bao lake la kufutia machozi katika dakika ya 76 mfungaji akiwa ni Jimmy Oyen ambaye aliingia kuchukua nafasi ya James Kun.
  Matokeo hayo yameiweka Azam FC kileleni mwa Kundi A ikiwa na pointi tatu na mabao mawili kwani katika mchezo wa kwanza wa kundi hilo uliochezwa uwanjani hapo leo mchana JKU ya Zanzibar imetoka sare ya bao 1-1 na Vipers ya Uganda.
  Katika nafasi ya pili ipo JKU ikiwa na pointi moja ikifuatiwa na Vipers pia yenye pointi moja.
  Bao la JKU lilifungwa na Salim Said Salim katika dakika ya 16 huku lile la Vipers likifungwa na mshambuliaji wa zamani wa Simba, Dan Sserunkuma dakika ya 29 baada ya kupokea pasi ya Milton Kaliisa.
  Kiungo wa JKU, Faisal Salum Abdallah ndiye aliyetwaa tuzo ya mchezaji bora wa mchezo huo.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: AZAM FC YAANZA VYEMA KOMBE LA KAGAME, YAICHAPA KATOR FC 2-1 MABAO YOTE KAFUNGA SHAABAN IDD CHILUNDA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top