• HABARI MPYA

  Jumanne, Juni 26, 2018

  BEKI MPYA MGANDA AAHIDI MATAJI AZAM FC, AGGREY MORRIS NA SURE BOY WATIWA PINGU HADI 2020

  Na Sada Salmin, DAR ES SALAAM
  BEKI mpya wa Azam FC, Mganda, Nicholas Wadada amewasili mjini Dar es Salaam leo kujiunga na mwajiri wake mpya huku akiahidi kuisadia timu kushinda mataji.    
  Mara baada ya kuwasili mchana wa leo, Wadada alisema; “Ninashukuru Mungu nimefika salama, nimekuja kuanza kazi Azam FC kwa matumaini makubwa, kwa kushirikiana na wenzangu nataka tuisaidie timu kushinda mataji,”.
  Beki huyo wa kulia na Nahodha wa kikosi cha wachezaji wa nyumbani wa The Cranes wiki iliyopita alisaini mkataba wa miaka miwili kujiunga na timu ya Alhaj Sheikh Said Salim Awadh Bakhresa na faimilia yake akitokea Vipers ya kwao.
  Usajili wake Azam FC ulizima tetesi kwamba Wadada aliyeng’ara katika Ligi Kuu ya Uganda alikuwa anatakiwa na klabu kadhaa za Afrika Kusini.

  Nicholas Wadada amewasili mjini Dar es Salaam leo kujiunga na Azam FC  

  Wadada mwenye umri wa miaka 23, amekuwa mchezaji wa timu ya taifa ya Uganda tangu mwaka 2012 na hadi sasa amekwishaichezea The Cranes mechi 46 na pamoja na kwamba ni mlinzi, lakini pia amefunga bao moja.
  Wadada anakuwa mchezaji mpya wa tatu wa kigeni kusajiliwa Azam FC kuelekea msimu mpya, baada ya Wazimbabwe, kiungo Tafadzwa Kutinyu kutoka Singida United na mshambuliaji Donald Ngoma kutoka Yanga.
  Lakini kwa ujumla, Wadada anakuwa mchezaji mpya wa tano kusajiliwa Azam FC kuelekea msimu ujao, kwani pamoja na Kutinyu na Ngoma, timu hiyo pia imewasajili wazawa kiungo Mudathir Yahya anayerejea nyumbani baada ya kucheza kwa mkopo Singida United msimu uliopita na Ditram Nchimbi kutoka Njombe Mji FC iliyoshuka Daraja.
  Ikumbukwe Azam FC msimu ujao itakuwa chini ya benchi jipya la Ufundi, Kocha Mkuu, Mholanzi Hans van der Pluijm kutoka Singida United na Msaidizi wake, mzalendo Juma Mwambusi ambao misimu miwili iliyopita walifanya kazi pamoja kwa mafanikio Yanga.
  Aggrey Morris (kulia) akisani mkataba wa kuendelea kuitumikia Azam FC hadi mwaka 2020. Kushoto ni Meneja Philipo Alando

  Salum Abubakar ‘Sure Boy’ (kulia) akitia dole gumba kusaini mkataba wa kuendelea kuitumikia Azam FC hadi mwaka 2020. Kushoto ni Meneja Philipo Alando

  Katika hatua nyingine, wachezaji wawili wazoefu, beki Aggrey Morris na kiungo Salum Abubakar ‘Sure Boy’ wameongeza mkataba wa kuendelea kuitumikia Azam FC hadi mwaka 2020.
  Kila mmoja wao alikuwa amebakiza mkataba wa mwaka mmoja na kwa kusaini leo mbele ya Meneja, Philipo Alando sasa watatumika Azam FC kwa miaka miwili ijayo.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: BEKI MPYA MGANDA AAHIDI MATAJI AZAM FC, AGGREY MORRIS NA SURE BOY WATIWA PINGU HADI 2020 Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top