• HABARI MPYA

  Jumapili, Juni 24, 2018

  BENZEMA AENDA NEW YORK BAADA YA KUTENGWA UFARANSA

  Na Mahmoud Zubeiry, aliyekuwa NEW YORK
  MSHAMBULIAJI wa Real Madrid, Karim Mostafa Benzema ameamua kwenda mapumziko Jijini New York, Marekani katika wakati huu wa fainali za Kombe la Dunia nchini Urusi.
  Benzema hayumo kwenye kikosi cha Ufaransa kinachoshiriki Fainali za Kombe la Dunia kutokana na msimamlo wa Rais wa Shirikisho la Soka Ufaransa (FFF), Noel Le Graet dhidi yake.
  Benzema hajachezea timu ya taifa ya Ufaransa tangu mwaka 2015 alipocheza dhidi ya Armenia kufuatia madai ya kutatanisha ya kutishia maisha yaliyomuhusisha mchezaji mwenzake, Mathieu Valbuena. 
  Benzema ameposti picha akifurahia maisha katika Jiji la New York nchini Marekani, wakati Ufaransa ikifanya vyema nchini Urusi na kujihakikishia mapema kwenda hatua ya 16 Bora baada ya kushinda mechi mbili mfululizo za kwanza za Kundi C.

  Karim Benzema ameposti picha akifurahia maisha New York, wakati Ufaransa ikifanya vyema nchini Urusi 

  Ameposti pia video akikatiza mitaa ya Jiji la New York kwa gari la kifahari huku shabiki wake mmoja akipanda juu ya gari na kuinua jezi yake. 
  Ufaransa iliyo chini ya kocha mzalendo, Didier Deschamps ilianza kwa kuichapa 2-1 Australia Juni 16 kabla ya kuilaza 1-0 Peru Juni 21 na itakamilisha mechi zake za Kundi C kwa kumenyana na Denmark Juni 26. 
  Tayari Benzema amekwishaichezea Ufaransa mechi 81 tangu mwaka 2007 na kuifungia mabao 27 na hiyo baada ya kuchezea timu za vijana kuanzia U17, U18, U19 na U21.
  Amekwenda mapumziko New York baada ya msimu mzuri akiwa na klabu yake, Real Madrid akiiwezesha kutwaa taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya kwa mara ya tatu mfululizo baada ya ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya Liverpool Uwanja wa Olimpiki mjini Kiev, Ukraine Mei 27. 
  Benzema alifunga bao la kwanza dakika ya 51 siku hiyo, kabla ya mshambuliaji Msenegali, Sadio Mane kuisawazishia Liverpool dakika nne baadaye na winga wa Wales, Gareth Bale kutokea benchi na kufunga mabao mawili dakika za 64 na 83. 
  Ikumbukwe ni Benzema alitoa mchango mkubwa kwa Real kwenda Fainali, baada ya kufunga mabao mawili dakika za 11 na 46 katika sare ya 2-2 na Bayern Munich kwenye mchezo wa marudiano wa Nusu Fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya Mei 2. 
  Mabao ya Bayern Munich siku hiyo yalifungwa na Joshua Kimmich dakika ya tatu na James Rodriguez dakika ya 63 na sasa Real Madrid inakwenda fainali kwa ushindi wa jumla wa 4-3, baada ya awali kushinda 2-1 Uwanja wa Allianz Arena mjini Munich, Ujerumani.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: BENZEMA AENDA NEW YORK BAADA YA KUTENGWA UFARANSA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top