• HABARI MPYA

  Jumamosi, Juni 23, 2018

  BOCCO AWABWAGA NYONI, OKWI TUZO YA MCHEZAJI BORA WA LIGI KUU

  Na Rehema Lucas, DAR ES SALAAM
  NAHODHA wa Simba SC, John Raphael Bocco ametwaa Tuzo ya Mchezaji Bora wa msimu uliopita wa Ligi Kuu ya Soka ya Vodacom Tanzania Bara usiku huu na kupata zawadi ya fedha ya Sh milioni 12.
  Katika sherehe za kukabidhi tuzo hizo zilizofanyika kwenye Ukumbi wa Mlimani City, Bocco amewashinda wachezaji wenzake wa Simba Erasto Nyoni na Emmanuel Okwi.
  Tuzo ya heshima imeenda kwa Edward Akwitende aliyeichezea Taifa Stars kati ya mwaka 1952 hadi 1954.
  Kikosi bora ni Aishi Manula wa Simba,  Hassan Kessy (Yanga), Shafique Batambuze (Singida United), Erasto Nyoni (Simba), Kelvin Yondani (Yanga), Pappy Kabamba Tshishimbi (Yanga), Shiza Kichuya (Simba), Tafadzwa Kutinyu (Singida United sasa yupo Azam FC), John Bocco (Simba), Emmanuel Okwi (Simba) na Marcel Kaheza wa Majimaji SC ambaye sasa amejiunga na Simba.
  John Bocco ametwaa tuzo ya mchezaji Bora wa Ligi Kuu Vodacom Tanzania Bara  

  Tuzo ya bao bora la msimu imeenda kwa Shaaban Idd wa Azam FC  akimshinda Seif Karie wa Lipuli FC. 
  Aliyeshinda tuzo ya Kocha Bora ni Kocha wa Abdallah Mohammed wa Prisons aliyewashinda Zuberi Katwila wa Mtibwa Sugar na Pierre Lechantre wa Simba. 
  Mwamuzi Bora Msaidizi imeenda kwa Hellen Mduma akiwashinda Mohammed Mkono na Ferdinand Chacha.
  Tuzo ya kipa bora imeenda kwa Aishi Manula wa Simba akiwashinda Aron Kalambo wa Prisons na Razack Abalora wa Azam FC. 
  Tuzo ya mwamuzi bora imeenda kwa Heri Sasii akiwashinda Jonesia Rukyaa na Hans Mabena. 
  Mchezaji bora Chipukizi imeenda kwa Habib Kiyombo wa Mbao FC ambaye amewashinda Shaban Idd na Yahya Zaid wote kutoka Azam FC. 
  Tuzo ya mchezaji anayechipukia yaani Tuzo ya Ismail Khalfan imeenda kwa Abuu Juma wa Mtibwa Sugar aliyepata Sh milioni nne akiwashinda Elia Nyondo wa Simba na Luichi Mwamba wa Mtibwa Sugar. 
  Timu yenye nidhamu ni Mtibwa Sugar ambayo imepewa Sh milioni 18 ikizishinda Simba na Kagera Sugar. 
  Tuzo ya mfungaji bora imeenda kwa Emmanuel Okwi wa Simba mwenye mabao 20 ambaye alipewa tuzo na fedha Sh Milioni 3. 
  Kwa timu zilizoshika nafasi mbalimbali katika nafasi ya nne Prisons imepata Sh milioni 27 Yanga katika nafasi ya tatu imepata Sh milioni 34 katika nafasi ya pili Azam FC imepata Sh milioni 48 na mabingwa Simba wamepata Sh milioni 96.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: BOCCO AWABWAGA NYONI, OKWI TUZO YA MCHEZAJI BORA WA LIGI KUU Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top