• HABARI MPYA

  Alhamisi, Juni 28, 2018

  MICHUANO YA KOMBE LA KAGAME KUANZA RASMI KESHO

  Na Rehema Lucas, DAR ES SALAAM
  MICHUANO ya soka ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Kagame itafunguliwa rasmi  kesho Ijumaa kwenye Uwanja wa Azam Complex uliopo Chamazi nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam.
  Michuano ya mwaka huu ya Kombe la Kagame inachezwa nchini baada ya mara ya mwisho kufanyika nchini pia mwaka 2015 ambapo Azam FC ilitwaa ubingwa kwa kuifunga Gor Mahia ya Kenya mabao 2-0.
  Katibu Mkuu wa Baraza la Vyama vya Soka Afrika Mashariki na Kati (CECAFA), ambao ndiyo waandaaji wa Kombe la Kagame, Nicolas Musonye amesema mpaka sasa wamejiandaa vizuri kufanikisha michuano hiyo.

  Kaimu Makamu wa Rais wa TFF, Athumani Nyamlani (katikati) akizungumza na Waandishi wa Habari. Kulia ni Ofisa Habari wa TFF, Clifford Ndimbo na kushoto Katibu wa CECAFA, Nicholaus Musonye

  “Kila kitu kipo sawa na kesho michuano hii tutaifungua rasmi na naamini tutafanya michuano bora na yenye wachezaji bora wanaoweza kupambana,” alisema Musonye.
  Musonye aliishukuru Azam TV kwa udhamini wake ikiwemo kuonyesha moja kwa moja mechi za Kombe la Kagame mwaka huu.
  Mkurugenzi wa Michezo wa Azam Media, Patrick Kahemele amesema wao wamejipanga vizuri kufanikisha michuano ya Kombe la Kagame ambayo itaanza kesho kwenye viwanja viwili vya Azam Complex na Taifa.
  Kaimu Makamu wa Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Athuman Nyamlani amesema wao kama TFF wamejiandaa ipasavyo kukamilisha michuano hiyo ya Kombe la Kagame.
  Kesho katika ufunguzi mechi za Kundi A ndizo zitakazokuwa za kwanza kuchezwa ambapo JKU ya Zanzibar itapambana na Vipers ya Uganda saa 8:00 mchana halafu itafuatiwa na mchezo wa Azam FC na Kator ya Sudan Kusini.
  Saa 1:00 usiku kwenye Uwanja wa Taifa, utachezwa mchezo wa Kundi C kati ya Singida United na APR ya Rwanda.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: MICHUANO YA KOMBE LA KAGAME KUANZA RASMI KESHO Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top