• HABARI MPYA

  Ijumaa, Juni 29, 2018

  SINGIDA UNITED YAIFUNGA APR MABAO 2-1 KATIKA KOMBE LA KAGAME USIKU TAIFA

  Na Sada Salmin, DARES SALAAM
  MUDA mfupi baada ya Azam FC kushinda mechi yake ya kwanza ya Kombe la Kagame, Singida United timu nyingine ya Tanzania imepata ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya APR ya Rwanda.
  Mchezo wa Singida United na APR umechezwa usiku huu kwenye Uwanja wa Taifa Dar es Salaam ukiwa wa kwanza wa Kundi C.
  Katika mchezo huo, mabao ya Singida United yamefungwa na Habib Kyombo dakika ya saba na bao la pili limefungwa na John Tiber katika dakika ya 82 akipiga kona iliyoenda moja kwa moja wavuni.
  Dakika ya 90 APR ilipata bao la kufutia machozi lililofungwa na Akizimana Muhadjil kwa kichwa akiunganisha mpira wa kona.

  Ushindi huo unaifanya Singida United ishike usukani wa Kundi C ikiwa na pointi tatu zikifuata Simba na Dakadaha ya Somalia ambazo kesho zitapambana kwenye Uwanja wa Taifa kuanzia saa 2:00 usiku.
  Katika michezo ya awali ya Kombe la Kagame leo mabingwa watetezi Azam FC wameanza vizuri harakati za kutetea ubingwa baada ya kuifunga Kator FC ya Sudan Kusini mabao 2-0.
  Mchezo huo uliochezwa kuanzia saa 11:00 jioni kwenye Uwanja wa Azam Complex uliopo Chamazi Mbagala jijini Dar es Salaam, mabao mawili ya Azam FC yalifungwa na mshambuliaji Shaaban Idd Chilunda.
  Chilunda aliifungia Azam FC bao la kwanza katika dakika ya 28, bao lililodumu hadi mapumziko na katika kipindi cha pili dakika ya 48 Chilunda alifunga bao la pili akipokea pasi ya Bruce Kangwa.
  Kator FC yenye wachezaji mchanganyiko kutoka Uganda na Kenya, ilipata bao lake la kufutia machozi katika dakika ya 76 mfungaji akiwa ni Jimmy Oyen ambaye aliingia kuchukua nafasi ya James Kun.
  Matokeo hayo yameiweka Azam FC kileleni mwa Kundi A ikiwa na pointi tatu na mabao mawili kwani katika mchezo wa kwanza wa kundi hilo uliochezwa uwanjani hapo leo mchana JKU ya Zanzibar imetoka sare ya bao 1-1 na Vipers ya Uganda.
  Katika nafasi ya pili ipo JKU ikiwa na pointi moja ikifuatiwa na Vipers pia yenye pointi moja.
  Bao la JKU lilifungwa na Salim Said Salim katika dakika ya 16 huku lile la Vipers likifungwa na mshambuliaji wa zamani wa Simba, Dan Sserunkuma dakika ya 29 baada ya kupokea pasi ya Milton Kaliisa.
  Michuano hiyo ya Kombe la Kagame inayoandaliwa na Baraza la Vyama vya Soka Afrika Mashariki na Kati (CECAFA) inaonyeshwa moja kwa moja na Azam TV. 
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: SINGIDA UNITED YAIFUNGA APR MABAO 2-1 KATIKA KOMBE LA KAGAME USIKU TAIFA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top