• HABARI MPYA

  Alhamisi, Juni 21, 2018

  CHALLENGE YA WANAWAKE SASA KUFANYIKA JULAI 19 HADI 29 RWANDA

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  MASHINDANO ya kuwania Kombe la Challenge Wanawake kwa nchi za Afrika Mashariki na Kati sasa yatafanyika kuanzia Julai 19 hadi 29 mwaka huu huko Rwanda.
  Awali mashindano hayo yanayoandaliwa na Baraza la Soka Afrika Mashariki na Kati (CECAFA) yalitarajiwa kufanyika Mei 12 hadi 22 mwaka huu lakini yalisongezwa mbele kutokana na sababu zisizozuilika.
  Katibu Mkuu wa CECAFA, Nicholas Musonye, amesema leo kwamba tayari maandalizi ya mashindano hayo ambayo yanafanyika kwa mara ya pili yameanza na taarifa kwenda kwa nchi wanachama zimeshapelekwa.

  Musonye alizitaja nchi ambazo zimethibitisha kushiriki mashindano hayo kuwa ni pamoja na wenyeji Rwanda, Kenya, Uganda, Djibouti, Zanzibar, Ethiopia na Kilimanjaro Queens kutoka Tanzania Bara ambao ndio mabingwa watetezi.
  Wakati huo huo, Musonye alitangaza rasmi kuzialika Singida United ya Tanzania Bara na APR ya Rwanda kuchukua nafasi zilizoachwa na Yanga pamoja na St.George ya Ethiopia ambazo zimejitoa kushiriki mashindano ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati maarufu Kombe la Kagame.
  "Kufuatia Yanga ya Tanzania na St. George kujitoa kwenye Kombe la Kagame, CECAFA imetulazimu kuziteua APR na Singida United kuchukua nafasi zao na vile vile kuirekebisha ratiba ya mashindano yetu," alisema Musonye ambaye kwa taaluma ni mwandishi wa habari.
  Aliongeza kuwa ratiba ya mechi za mashindano hayo zimezingatia na haitaingiliana na mechi za michuano ya Kombe la Dunia ambayo inaendelea Urusi.
  Azam FC ndio mabingwa watetezi wa mashindano hayo ambayo bingwa wake atapata zawadi ya Dola za Marekani 30,000 wakati mshindi wa pili ataondoka na Dola za Marekani 20,000 huku timu itakayomaliza katika nafasi ya tatu itajinyakulia Dola za Marekani 10,000.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: CHALLENGE YA WANAWAKE SASA KUFANYIKA JULAI 19 HADI 29 RWANDA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top