• HABARI MPYA

  Ijumaa, Juni 29, 2018

  ROONEY ATAMBULISHWA DC UNITED NA KUKABIDHIWA JEZI NAMBA 9

  Na Mahmoud Zubeiry, WASHINGTON
  HATIMAYE mshambuliaji wa zamani wa kimataifa wa England, Wayne Rooney ametambulishwa katika klabu yake mpya D.C. United baada ya kuwasili leo jioni.
  Rooney anayetokea Everton ya kwao, England ameposti picha akiwa na jezi ya DC United na video ya tangazo la utambulisho wake na kuthibitisha atacheza mechi yake ya kwanza Julai 14 dhidi ya Vancouver Whitecaps Uwanja mpya wa Audi Field.
  Mapema leo, gazeti la Washington Post lilisema kwamba Rooney mwenye umri wa miaka 32 atakuwa mchezaji ghali zaidi atakaposaini mkataba wa miaka miwili na nusu ambao atalipwa dola za Kimarekani Milioni 13.
  Rooney anatarajiwa kuanza mazoezi na timu yake mpya mwishoni mwa wiki hii, kwa mujibu wa gazeti la Post, ambalo limeripoti pia kwamba tayari amepatiwa kibali cha kuishi na kufanya kazi Marekani na anatarajiwa kucheza mechi ya kwanza Uwanja mpya wa Audi Field Julai 14 dhidi ya Vancouver Whitecaps.

  Wayne Rooney ametambulishwa katika klabu yake mpya D.C. United baada ya kuwasili leo jioni

  D.C. United inahitaji msaada, kwani kwa sasa inashika mkia kwenye Ligi ya MLS Kanda ya Mashariki ikiwa imekusanya pointi 10 tu katika mechi 12 na kocha Ben Olsen amesema Rooney anaweza kuwasaidia kupanda.
  Msimu uliopita Rooney alichezea klabu yake iliyomuibua utotoni, Everton akitokea Man United alikoondoka katikati ya mwaka 2017 na kuifungia Toffees mabao 11 katika mechi 40 za mashindano ikimaliza nafasi ya nane Ligi Kuu.
  Rooney alibakiza mwaka mmoja katika mkataba wake Everton, lakini klabu hiyo imeshindwa kupambana na msimamo wa mfungaji huyo wa kihistoria wa mabao wa timu ya taifa ya England kuhamia Marekani.
  Rooney alisaini Man United mwaka 2004, akitokea Everton kijana mdogo wa umri wa miaka 18 kwa dau la Pauni Milioni 25.6 na kwenda kuifungia klabu hiyo jumla ya mabao 253 katika mechi 559 Uwanja wa Old Trafford, akishinda mataji matano ya Ligi Kuu ya England.
  Rooney, anayeshika nafasi ya tano katika orodha ya wachezaji waliocheza mechi nyingi Man United kihistoria, pia ameshinda mataji ya Ligi ya Mabingwa Ulaya, Europa League, Kombe la FA na Kombe la Ligi mara tatu katika miaka yake 13 ya kuwatumikia Mashetani hao Wekunfu.
  Rooney amestaafu timu ya taifa ya England, ijulikanayo kama ‘Simba Watatu’ akiwa ameichezea mechi 119 na kuifungia 53.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: ROONEY ATAMBULISHWA DC UNITED NA KUKABIDHIWA JEZI NAMBA 9 Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top