• HABARI MPYA

  Jumatano, Juni 20, 2018

  KIPA WA ZAMANI WA PAMBA, PAUL RWECHUNGURA AELEZEA FAIDA ZA URAIA WA NCHI MBILI KWA SEKTA YA MICHEZO

  Na Mahmoud Zubeiry, PHILADELPHIA
  KIPA wa zamani wa klabu ya Pamba ya Mwanza, Paul Gervas Rwechungura amesema kwamba siku Tanzania ikiruhusu uraia wa nchi mbili wanamichezo wengi waliozaliwa nje watajitokeza kutaka kuiwakilisha nchi yao ya asili.
  Rwechungura ameyasema hayo katika mahojiano maalum na Bin Zubeiry Sports – Online leo mjini hapa wakati akitoa maoni yake juu ya kijana Yussuf Poulsen kuchezea timu ya taifa ya Denmark japokuwa asili yake ni Tanga.
  Kwanza Rwechungura ameunga mkono wazo la Mkurugenzi wa Michezo Dk. Yusuph Singo aliyeshauri kuwe na utaratibu maalum wa kuwatambua wanamichezo wenye asili ya Tanzania wanaocheza nje.
  Lakini Rwechungura akasema hiyo haitoshi kama wanamichezo hawatapewa masharti nafuu ya kuziwakilisha nchi zao za asili, ikiwemo kuwa na uraia wa nchi mbili kama ilivyo kwa nchi nyingine za Afrika, zikiwemo jirani za Kenya na Uganda.

  Paul Rwechungura amesema Tanzania itavuna wanamichezo wengi kutoka nje ikiruhusu uraia wa nchi mbil
  Paul Rwechungura akiidakia Pamba FC dhidi ya Simba SC mwaka 1990 
  Paul Rwechungura akiidakia Pamba FC dhidi ya Yanga mwaka 1991
  Paul rwechungura katika kikosi cha Pamba FC mwaka 1991 Uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam kabla ya mechi na Yanga

  “Amini nakuambia, siku Tanzania itakapopitisha sheria ya uraia wa nchi mbili watajitokeza wanamichezo wengi wa kuiwakilisha nchi yetu ambao wana asili nayo,”.
  “Watanzania wengi wameondoka Tanzania na wapo nchi mbalimbali duniani huko wamepata familia na wengine wana watoto ambao ni wanamichezo wazuri, mfano huyo Yussuf Poulsen,”. 
  “Hata mimi wanangu wanacheza hapa Marekani, wanafanya vizuri kwenye michezo ya vyuo, lakini wana uhuru wao wa kuchagua kufuata uraia wangu, au wa walipozaliwa (Marekani). Lakini naamini wanaipenda nchi yao, wakijua hawatapoteza haki zao za kuwa Wamarekani wakiiwakilisha nchi yao ya asili, wanaweza kuja kuchezea Tanzania,”amesema.
  Rwechungura yupo Marekani tangu mwaka 1994 anakoishi na familia yake baada ya kustaafu soka kufuatia kuchezea timu za RTC Kagera ya Bukoba, Pamba ya Mwanza na Maji Maji ya Songea nchini Tanzania.
  Klabu yake ya mwisho ni Philadelphia Union ya hapa Marekani aliyoichezea mwaka 1994 hadi 1995 kabla ya kustaafu na kwenda kujiendeleza kielimu.      
  Hoja ya uraia wa nchi mbili iligonga mwamba mwaka 2014 kwenye Bunge la Katiba, baada ya Wajumbe kujiridhisha itakuwa na hasara kubwa kuliko faida, hofu kubwa iliyojitokeza ni watu kuchuma mali nyumbani na kuhamishia fedha nje.
  Lakini upande wa pili, wapenzi wa michezo wameendelea kuipigia debe kwa imani kwamba watoto wa Watanzania waishio nje ambao wanacheza na kufanya vizuri wanaweza kuja kuisaidia nchi yao ya asili.
  Na hivi karibuni suala hilo limeibuka tena, baada ya kijana Poulsen kuibukia kwenye kikosi cha timu ya taifa ya Denmark kwenye fainali za kombe la Dunia zinazoendelea nchini Urusi.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: KIPA WA ZAMANI WA PAMBA, PAUL RWECHUNGURA AELEZEA FAIDA ZA URAIA WA NCHI MBILI KWA SEKTA YA MICHEZO Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top