• HABARI MPYA

  Jumatatu, Juni 25, 2018

  NTEZE JOHN: TANZANIA INAHITAJI WACHEZAJI WENGI WANAOCHEZA ULAYA ILI KUWA TIMU BORA YA TAIFA

  Na Mahmoud Zubeiry, SEATTLE
  MSHAMBULIAJI wa zamani wa kimataifa wa Tanzania, Nteze Johnson John Lungu amesema kwamba nchi inahitaji kuwa na wachezaji wengi wanaocheza ligi mbalimbali barani Ulaya ili kuwa na timu bora ya taifa.
  Katika mahojiano maalum na Bin Zubeiry Sports – Online leo mjini hapa, Nteze au Johnson kwa jina la ubatizo, amesema kwamba lazima zifanyike jitihada za makusudi kuhakikisha vijana wa Kitanzania wanapata nafasi kwa wingi kucheza Ulaya.
  “Mimi siwezi kusema wafanye nini, ni jukumu la watu waliopewa dhamana hapo nyumbani kuongoza mpira wetu kuanzia kwenye klabu na TFF (Shirikisho la Soka Tanzania) kuhakikisha wanafanikisha hilo, lakini kwanza lazima tutengeneza wachezaji kuanzia ngazi ya chini kabisa,”amesema.

  Nteze John katika mahojiano maalum na Bin Zubeiry Sports – Online jana mjini Seattle, Marekani 

  Nteze John (wa pili kushoto waliosimama) akiwa katika kikosi cha timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars mwaka 1994


  Nteze John (wa pili kulia waliopiga magoti) akiwa katika kikosi cha klabu ya Simba mwaka 1994

  Nteze ameshauri viongozi wa TFF na klabu watoke na kwenda kujifunza Ulaya, Amerika, Asia na hata baadhi ya nchi za Afrika zilizofanikiwa kisoka kuhusu programu za vijana zinavyoendeshwa.
  “Lazima viongozi wetu kuanzia wa klabu wajue namna ya kuendesha hizi programu za vijana kwa kujitoa kwenda kujifundisha kwa wenzetu waliofanikiwa. Ukisikia propgamu za vijana si kuwa na timu za vijana tu, bali wanalelewa vipi, wanakuzwa vipi hadi kwenye kuwa wachezaji kamili, hayo ndiyo mambo ya kujifunza ili kusudi tuache kufanya vitu kwa kudhani na mazoea,”amesema.
  Aidha, Nteze amewashauri wachezaji wa Tanzania wanaofanya vizuri kwa sasa na ambao wapo katika timu ya taifa kuhangaika wenyewe kutafuta nafasi za kwenda kucheza nje.
  “Wakati wetu sisi tunacheza tulikuwa na changamoto ya kuzuiwa kwenda nje, wengi wetu nikiwepo mimi tulipoteza nafasi nyingi sana za kucheza nje kutokana na kubaniwa na viongozi. Ila kwa sasa naona haya mambo yamepungua na vijana wanaruhusiwa, basi waitumie fursa hiyo vizuri,”amesema.
  Baada ya kustaafu soka mwaka 2004 kufuatia kuzichezea timu za Pamba ya Mwanza, Simba SC, Kajumulo WS za Dar es Salaam, Qwa Qwa Stars, sasa Free State Stars ya Afrika Kusini, Persikaba FC ya Indonesia na Sun Heung FC ya Hong Kong Nteze kwa sasa anaishi Jijini Seattle, Marekani tangu mwaka 2005 na familia yake. 
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: NTEZE JOHN: TANZANIA INAHITAJI WACHEZAJI WENGI WANAOCHEZA ULAYA ILI KUWA TIMU BORA YA TAIFA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top